Pata taarifa kuu
DRC-UCHAGUZI

DRC: Maandamano ya upinzani yakosa uungwaji mkono

Ofisi ya chama kikuu cha upinzani nchini DRC, UDPS
Ofisi ya chama kikuu cha upinzani nchini DRC, UDPS RFI/Habibou Bangré

Maandamano yaliyoitishwa Jumanne hii na viongozi wa upinzani nchini DRC yameshindwa kupata muitikio mkubwa kama ilivyotarajiwa baada ya Serikali kuyapiga marufuku na kusambaza maelfu ya polisi.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani ulikuwa unajaribu kuwashawishi wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kwenye viunga vya jiji la Kinshasa na maeneo mengine ya nchi kushinikiza rais Joseph Kabila kuondoka madarakani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Maandamano haya yalikuwa yanalenga pia kupinga kalenda mpya iliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini DRC CENI ambayo sasa inaonesha kuwa uchaguzi mkuu utafanyika Desemba 23 mwaka 2018.

Rais Kabila alikuwa amemaliza muda wake Desemba 20 mwaka jana kabla ya kufikiwa kwa makubaliano kati ya baraza la maaskofu wa kanisa katoliki CENCO na wanasiasa kuwa uchaguzi ungefanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Upinzani umeendelea kushinikiza kuwa unataka kuundwa kwa Serikali ya mpito bila ya rais Kabila kuanzia Januari Mosi mwaka 2018.

Gavana wa jiji la Kinshasa tayari alikuwa amewaonya wanasiasa wa upinzani kutoka chama cha UDPS dhidi ya maandamano yao aliyosema haya uhalali kwa kuwa tume ya uchaguzi ilishatangaza tarehe ya uchaguzi.

Wito wa maandamano uliokuwa umetolewa na upinzani ulisababisha shughuli kupungua katikati ya jiji la Kinshasa ambapo kinyume na ilivyokawaida hakukuwa na msongamano wa magari wala watu kama ilivyozoeleka.

Ulinzi mkali uliwekwa kuzingira jiji la Kinshasa na njia ya kuelekea kwenye makazi ya kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi.

Watu waliojaribu kuandamana kwenye miji ya Bukavu, Mbuji Mayi Kasai ya Kati walishindwa kufanya hovyo kwa hofu ya kukamatwa na Polisi.

Mjini Goma maandamano hayakufanyika kabisa kutokana na ulinzi uliokuwa umewekwa tangu Jumatatu kufuatia mkutano unaoendelea wa magavana 26, mkutano ambao unahudhuriwa pia na rais Joseph Kabila.

Mamia ya watu walipoteza maisha katika maandamano ya mwezi Septemba mwaka 2016 na mwezi Desemba mwaka jana jijini Kinshasa ambapo maelfu ya raia waliandamana kushinikiza kuondoka madarakani kwa rais Kabila wakati muda wake utakapomalizika mwezi Desemba mwaka jana.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.