Pata taarifa kuu
AFRIKA-ASIA-AMERIKA-ULAYA-WAKIMBIZI-HAKI

Siku ya Wakimbizi Duniani yaadhimishwa

Kambi ya wakimbizi kutoka Mali nchini Mauritania
Kambi ya wakimbizi kutoka Mali nchini Mauritania © Reuters

Ulimwengu unaadhimisha Jumatano wiki hii Siku ya Wakimbizi Duniani. Siku hii inaadhimishwa wakati ambapo idadi ya wakimbizi inaendelea kuongezeka.

Matangazo ya kibiashara

Idadi ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao kufuatia migogoro duniani imefikia hadi zaidi ya milioni 68.5, karibu nusu yao ikiwa ni watoto, Umoja wa mataifa ulisema Jumanne wiki hii.

Siku ya Wakimbizi Duniani inayoadhimishwa tarehe 20 Juni kila mwaka, ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2000 kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mkataba wa utambuzi wa hadhi ya wakimbizi ulipotiwa mkwaju kunako mwaka 1951, baada ya Jumuiya ya Kimataifa kujionea athari za Vita kuu ya Pili ya Dunia. Siku hii ikaanza kuadhimishwa rasmi mwaka 2001.Takwimu zinaonesha kwamba, leo hii kuna idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kuliko wakati mwingine wowote wa historia ya mwanadamu.

Katika Hotuba yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema idadi hiyo ni sawa na idadi ya watu kwenye nchi ya 20 kwa ukubwa zaidi duniani. “Mwaka jana, katika kila sekunde mbili mtu mmoja alikimbia makazi. Hasa katika nchi maskini zaidi,” amesema Guterres.

Kwa mantiki hiyo katika siku ya Wakimbizi Duniani, hii leo anasema ni “lazima tufikirie tufanye nini zaidi ili kusaidia. Jibu linaanza na umoja na mshikamano.”

Bwana Guterres anasema katika dunia ya leo jamii au nchi ambayo inayotoa hifadhi salama kwa wakimbizi wanaokimbia vita au mateso hawapaswi kuachwa peke  yao bila kusaidiwa.

Amepigia chepuo mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi utakaowasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baadaye mwaka huu akisema unatoa mwelekeo wa mbele na kutambua michango ya wakimbizi katika jamii zinazowahifadhi.

“Alimradi kuna vita na mateso, wakimbizi wataendelea kuwepo.   Katika siku ya Wakimbizi Duniani, nakuomba uwakumbuke. Simulizi zao ni za mnepo, uvumilivu na ujasiri. Zetu zinapaswa kuwa za mshikamano, upendo na vitendo.” Amehitimisha Katibu Mkuu.

Siku ya Wakimbizi Duniani huadhimishwa tarehe 20 mwezi Juni. Siku hiyo iliundwa mnamo mwaka wa 2000 na azimio maalum la mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Tarehe 20 mwezi Juni hapo awali ilikuwa ikiadhimishwa kama Siku ya Wakimbizi wa Afrika katika nchi kadhaa za Kiafrika.

Nchini Uingereza Siku ya Wakimbizi Duniani huadhimishwa kama sehemu ya Wiki ya Wakimbizi. Wiki ya Wakimbizi ni tamasha la kitaifa lilioundwa ili kukuza uelewano na kusherehekea mchango wa kitamaduni wa wakimbizi, na huhusisha matukio mengi kama vile muziki, ngoma na maigizo.

Katika Kanisa Katoliki, Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani huadhimishwa kila mwezi Januari kuanzia mwaka 1914, ilipoanzishwa na Papa Pius X.

“Hakuna Chochote” ni wimbo wa kiutamaduni wa Bob Thomas na Huw Pudner kuhusu shida ya mkimbizi anayelazimishwa kurudi nchi yake ya kiasili kinyume na nia yake.

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018  unaondaliwa na Umoja wa Mataifa unalenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Umuhimu wa Jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine, kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na wakimbizi kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao pamoja na  uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka!

Idadi ya wakimbizi duniani inatisha

Shirika la UNHCR, linasema idadi ya wakimbizi imeongezeka duniani na kuwa kubwa zaidi kushuhudiwa tangu vita vya pili vya dunia.

Wadadisi wanasema “kuna umuhimu wa Serikali husika kulinda mipaka ya nchi yake na kuratibu wimbi la wakimbizi na wahamiaji, lakini pia inapaswa kuwa na mfumo bora wa sheria unaoratibu na kusimamia shughuli za wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia: utu wao kama binadamu na haki zao msingi, kipaumbele cha kwanza wakiwa ni wanawake, watoto na wazee. Hapa sheria, mikataba na itifaki za kimataifa hazina budi kuzingatiwa na vyombo vya sheria katika nchi husika.”

Yaelezwa kuwa hadi sasa zaidi ya watu milioni 68 ni wakimbizi ugenini au ndani ya nchi zao, sababu kuu ikiwa ni mizozo au mateso kwenye nchi zao.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.