Pata taarifa kuu
AFRIKA-UCHUMI-BIASHARA-CAMEROON

Watalaam: Afrika inaelekea pazuri kujikomboa kiuchumi

Watalaam kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika  wanaohudhuria kongamano kuhusu biashara na uchumi lililoandaliwa na Umoja wa Afrika, jijini Yaounde nchini Cameroon, 06 Machi 2019
Watalaam kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wanaohudhuria kongamano kuhusu biashara na uchumi lililoandaliwa na Umoja wa Afrika, jijini Yaounde nchini Cameroon, 06 Machi 2019 Emmanuel Makundi

Wataalamu wa umoja wa Afrika wanasema kuwa bara hilo linaelekea pazuri katika kujikomboa kiuchumi kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na mataifa mbalimbali kurekebisha hali za uchumi wao.

Matangazo ya kibiashara

Haya yamesemwa katika mkutano wa kiufundi wa mawaziri wa fedha, uchumi, mipango na ushirikiano wa kikanda unaoendelea mjini Yaoundé, Cameroon.

Akizungumza na idhaa ya Kiswahili ya RFI, mtaalamu wa masuala ya Sera za uchumi na utafiti kutoka umoja wa Afrika, Dr. Ligane Msene, amesema kwa sasa nchi za Afrika zimeonesha kupiga hatua kubwa katika mchakato wa uanzishaji wa viwanda hali iliyochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa kutoka barani Afrika.

“Ukiangalia sio rahisi kuona hatua zilizopigwa lakini Afrika imepiga hatua katika mchakato wa viwanda, sababu kwa leo idadi ya vitu vilivyotengenezwa barani Afrika imeongezeka”.

Dr Sene amesema maendeleo haya yamechangiwa pakubwa na kukua kwa teknolojia, ambapo nchi wanachama zimeanza kuona umuhimu wake katika kujikwamua kiuchumi na kuongeza kasi ya uzalishaji.

Sene ameongeza kuwa kupanuka kwa teknolojia ya mawasiliano pia kumechangia pakubwa kurahisisha muingiliano wa nchi na nchi jambo ambalo limesaidia pakubwa kuchochea azma ya umoja wa Afrika ya kuwa na ushirikiano imara wa kikanda na kufanya biashara baina ya nchi wanachama.

“Maendeleo haya yametokana na kuimarika kwa mfumo wa kidigitali barani Afrika, lakini pia kutokana na ongezeko la washirika wa kibiashara, ambapo sasa Afrika inafanya biashara na wachina, wahindi jambo ambalo litaimarisha teknolojia kiasi kwamba bidhaa kutoka barani Afrika zitakuwa na uwezo wa kushindana na bidhaa za mataifa mengine katika soko”.

Kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya uzalishaji ni suala jingine ambalo Dr. Sene amesisitiza na kwamba kuongeza kasi ya ushirikiano wa kikanda ni hatua ya kwanza katika kutengeneza fursa ya kupanua masoko kwa makampuni mengi zaidi barani Afrika ili kusambaza bidhaa zao nje.

Kuhusu janga la wahamiaji hasa vijana wanaotoka barani Afrika kwenda Ulaya kutafuta maisha, Dr Sene amesema ni lazima kwa bara litofautishe sababu zinazowafanya vijana kuamua kupanda meli kwenda Ulaya kupitia njia ambazo si salama na zinazohatarisha maisha yao.

Dr. Sene amesema sababuj kubwa inayowashawishi vijana kukimbia nchi zao ni hali ya uchumi wa mataifa yao pamoja na ukosefu wa ajira, mambo ambayo amesema yanaweza kutatuliwa kwa nchi wanachama kutengeneza mazingira bora ya ajira na kuboresha hali ya maisha ya raia wake ili waweze kusalia na kufanya kazi kwenye nchi zao.

“Kwangu mimi nafikiri inabidi kukabiliana na sababu maalum ya watu kuhama ambapo sababu kubwa ni maendeleo hasi na ukosefu wa ajira kwa vijana hao”.

Mtaalamu huyo ameongeza kuwa bara la Afrika linazo rasilimali nyingi kama vile gesi, mafuta na madini, rasilimali ambazo amesema ikiwa zitatumika kwa uaminifu zinaweza kubadilisha kabisa taswira ya bara la Afrika kiuchumi.

Amesema imefika wakati ambapo viongozi wa Afrika waamue na kutambua utajiri mkubwa ambao bara hilo linao kwaajili ya kubadili maisha ya raia wake.

Katika mkutano huu, wajumbe karibu wote wamekubaliana kuharakisha mchakato wa upitishaji miradi ya maendeleo kwa bara la Afrika huku wakisisitiza suala la utawala na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, mambo ambayo wamesema yanakwamisha bara la Afrika kupiga hatua.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.