Pata taarifa kuu
MISRI-MORSI-MAZISHI-SIASA-KIFO

Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi azikwa jijini Cairo

Aliyekuwa rais wa Misri Mohamed Mursi wakati akiwa hai, akiwa Mahakamani
Aliyekuwa rais wa Misri Mohamed Mursi wakati akiwa hai, akiwa Mahakamani REUTERS

Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi amezikwa jijini Cairo, baada ya kuzirai na kufariki dunia akiwa Mahakamani siku ya Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Wakili wake ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa, kiongozi huyo wa zamani amezikwa Mashariki mwa jiji la Cairo, mazishi yaliyohudhuriwa tu na familia yake.

Aidha, mtoto wake wa kiume Abdullah Mohamed Morsi, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa, serikali ya Misri ilizuia ombi la familia la kutaka Morsi kuzikwa alikozaliwa na wananchi kuruhusiwa kuhudhuria.

Morsi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 67 na alikuwa anazuiwa jela akishtakiwa na makosa mbalimbali baada ya kuondolewa madarakani mwaka 2013.

Watetezi wa Haki za binadamu wakiongozwa na Shirika la Human Rights Watch, wamelaani mazingira mabaya na magumu ambayo Morsi alikuwa anazuiwa na wametaka uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu kifo hicho.

Kabla ya kifo chake wanaharakati na familia yake, walikuwa wanalamikia Morsi kutopata huduma nzuri ya matibabu na kuzuiwa kwa saa nyingi, na hata kuzuiwa kuonana na wapendwa wake.

Kundi la Muslim Brotherhood na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, mshirika wa karibu wa Morsi ameilamu serikali ya Misri kwa kusababisha kifo hicho.

Morsi alikuwa rais wa tano wa Misri aliyechaguliwa kidemokrasia baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa zamani, Hosni Mubarak mwaka 2012.

Aliongoza nchi hiyo ya Afrika Kaskazini kati ya tarehe 30 Juni 2012 hadi tarehe 3 mwezi Julai 2013 kabla ya kuondolewa madarakani na jeshi likiongozwa na rais wa sasa Jenerali Abdel Fattah el-Sisi.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.