Pata taarifa kuu
VENEZUELA-SIASA-HAKI

Venezuela: Serikali ya Maduro kuanzisha uchunguzi dhidi ya Juan Guaido

Mwanasheria Mkuu Tarek William Saab (akiwa mbele), Caracas, Januari 29, 2019.
Mwanasheria Mkuu Tarek William Saab (akiwa mbele), Caracas, Januari 29, 2019. REUTERS/Manaure Quintero

Serikali ya Nicolas Maduro imeanzisha mbinu mpya ya kukabiliana na kiongozi mkuu wa upinzani, Spika wa bunge la nchi hiyo Juan Guaido, ambaye hivi karibuni amejitangaza kuwa ni rais wa mpito wa Venezuela.

Matangazo ya kibiashara

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tarek William Saab, mshirika wa karibu wa Nicolas Maduro, ameanzisha uchunguzi dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani. Bw Saab ameomba Mahakama Kuu (TSJ), taasisi iliyo mikononi mwa Nicolas Maduro, kupiga marufuku Juan Guaido kuondoka nchini Venezuela na kuzuia akaunti zake za benki.

Hivi karibuni Bw Guaido alitoa wito wa kufanyika kwa maandamano mapya leo Jumatano na Jumamosi kwa lengo la kushinikiza jeshi, linaloendelea kumtii rais aliyechaguliwa Nicolas Maduro, na kuunga mkono onyo la Ulaya kwa ajili ya uchaguzi huru.

"Jumatano kuanzia saa sita hadi saa nane mchana, nchini kote Venezuela tutamiminika mitaani (...) kuomba jeshi la nchi kuunga mkono madai ya wananachi, na Jumamosi (tunatoa wito) wa kufayika kwa maandamano kubwa nchini Venezuela na kwingineko duniani kuunga mkono onyo la Umoja wa Ulaya, "alisema Juan Guaido, Spika wa bunge la venezuela, mwenye umri wa miaka 35.

Siku ya Jumamosi nchi sita za Ulaya (Uhispania, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Ureno, Uholanzi) zilimpa Nicolas Maduro muda wa siku nane kuitisha uchaguzi, la sivyo zitamtambua Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela. Muda huo utatamatika siku ya Jumapili.

Tayari Marekani na nchi kadhaa za Amerika Kusini zimetangaza kuwa zinamtambuwa Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela.

Kwa upande wa kimataifa, nchi ndogo zinamuunga mkono Nicolas maduro, ikiwa ni pamoja na China, Uturuki, Mexico na Urusi.

Hata hivyo Juan Guaido ameendelea kupokea uungwaji mkono.

Siku ya Alhamisi jioni alitangaza kwamba anataka kuandaa haraka uchaguzi mpya.

Hivi karibuni Waziri wa Ulinzi, Jenerali Vladimir Padrino, alionekana katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi wiki hii huko Caracas akizungukwa na uongozi wa jeshi katika ngazi ya juu ili kulaani "jaribio la mapinduzi" lililofanywa na spika wa Bunge.

"Ninatoa tahadhari kwa raia wa Venezuela kwamba jaribio la mapinduzi limefanywa dhidi ya taasisi za uongozi wa nchi, dhidi ya demokrasia, dhidi ya Katiba yetu, dhidi ya Rais Nicolas Maduro, rais wetu halali," alisema waziri huyo.

Awali Majenerali wanane ambao wanaongoza Majimbo muhimu ya nchi hiyo walisema bado "wanamtii" Rais Nicolas Maduro, katika ujumbe uliorushwa kwenye televisheni ya serikali.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.