Pata taarifa kuu
UFARANSA-TANZANIA

Wanafunzi Afrika Mashariki watangaziwa fursa za kusoma Ufaransa

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier YouTube Crop

Nchi ya Ufaransa imeendelea kukita mizizi yake kwenye nchi za Afrika Mashariki ambapo safari hii imeanza kuvutia wanafunzi kutoka kwenye nchi za ukanda kwenda kusoma katika vyuo vikuu vyake.

Matangazo ya kibiashara

Hatua ya Ufaransa imekuja baada ya mwezi Machi mwaka huu akiwa ziara nchini Kenya, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutangaza fursa za masomo kwa wanafunzi kutoka barani Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, balozi wa Ufaransa nchini humo, Frederic Clavier, amesema mpango huu uliotangazwa na rais Macron unalenga kuvutia zaidi ya wanafunzi nusu milioni kutoka mataifa ya kigeni hadi kufikia mwaka 2027.

“Ili kufikia lengo hili, ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania mwezi uliopita ulizindua mpango mpya kwa kufungua vituo vitatu vya taarifa kuhusu fursa za kwenda kusoma Ufaransa chini ya mwavuli wa Cumpus France, kwa upande wa Dar es Salaam na Zanzibar”.

Frederic Clavier Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania PAD

Balozi Clavier amesema kwa sasa nchi ya Ufaransa ina jumla ya wanafunzi laki 3 na elfu 32 wanaosoma kwenye vyuo vya Ufaransa.

Akizungumza katika hafla ya kwanza iliyowakutanisha na kutambua kuanzishwa kwa mtandao wa wanafunzi waliosoma Ufaransa, balozi Clavier amesema “hii ni fursa ambayo wanafunzi wa Tanzania wanapaswa kuitumia”.

Balozi Clavier pia akatangaza kuwa kwa mara ya kwanza nchi yake na Tanzania zitaandaa maonesho ya kimataifa ya elimu ya juu yatakayofanyika Desemba 14 mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa wa mwalimu Nyerere.

“Ufaransa iko tayari kufungua milango yake na kutoa fursa kwa wanafunzi wa kiafrika kusoma programu mbalimbali Ufaransa na hasa wanafunzi kutoka Afrika Mashariki”.

Aidha amesema wanafunzi wa Tanzania na nchi za ukanda hawapaswi kuogopa kuomba ufadhili wa kwenda kusoma Ufaransa wala kufikiria lugha kuwa kikwazo kwa kuwa sasa wanaweza kusoma kwa kutumia lugha ya kingereza.

“Mpaka kufikia mwishoni mwaka mwaka 2019, zaidi ya programu elfu 1 zitafunmdishwa kwa lugha ya kiingereza, nyingi zikiwa ni programu za uzamivu”.

Katika Kufanikisha hili Ufaransa imeanzisha tovuti maalumu ambayo wanafunzi wanaweza kuitumia kwa kujisajili na kupata fursa ya kujua nafasi za ufadhili zilizopo pamoja na fursa za ajira kutoka kwa makampuni yake ambayo mengi hivi sasa yamewekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki.

Katika hafla hiyo walikuwepo wanafunzi wanaotarajiwa kwenda kusoma Ufaransa kuanzia mwezi ujao na wale ambao walisoma Ufaransa kwa nyakati tofauti.

Boza Bonifansia ni mmoja wa wanafunzi walionufaika na ufadhili wa kwenda kusoma Ufaransa ambapo alisomea masomo ya E-business na sasa amerejea nyumbani na kujiajiri.

Boza Bonifansia Kijana aliyepata nafasi ya Kusoma Ufaransa

“Napenda nishukuru Ubalozi kwa kutoa fursa kama hizi, kwangu mimi ilikuwa ni fursa ya kipekee, nilijifunza namna ambavyo wenzetu wanaandaa programu zao jambo ambalo nimeona ni tofauti kabisa na namna vyuo vyetu vinafundisha.”

“Nawashauri wale waliopata nafasi ya kwenda, mkakaze buti kweli kweli kwani msuli wa kule sio wa kitoto,” alisema Boza.

Kwa upande wake muhadhiri msaidizi kutoka chuo kikuu cha elimu DUCE, Israel Monday ambaye pia ndie rais wa kwanza wa “Mtandao wa wanafunzi waliosoma Ufaransa”, amesema jukwaa hili litatoa fursa nyingi zaidi kwa watanzania kwenda kusoma Ufaransa.

Israel Monday Mhadhiri Msaidizi DUCE

“Mimi nilipata nafasi ya kwenda kusoma Ufaransa wakati fulani, nimejifunza namna wenzetu wanavyothamini elimu, hata hivyo kiwango cha elimu kinachotolewa na vyuo vya Ufaransa ni ya kiwango cha juu sana.”

“Nawashauri wanafunzi walioko kwenye vyuo vikuu kujisajili kupitia tovuti maalumu, huko watapata kujua mengi ikiwa ni pamoja na fursa za ufadhili na hata nafasi za kazi za makampuni ya Ufaransa’.

Monday amesema kwa sasa suala la Lugha sio kikwazo tena kwa wanafunzi kwa kuwa programu nyingi sasa zinafundishwa kwa lugha ya kingereza.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.