Pata taarifa kuu
FIFA-KOMBE LA DUNIA

Infantino: Afrika itapata nafasi zaidi ya 7 kwenye mpango wa nyongeza ya timu 48 kombe la dunia lijalo

Rais wa Fifa, Gianni Infantino.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino. Reuters

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani, fifa, Gianni Infantino, amethibitisha kuwa bara la Afrika litapata nafasi zaidi ya 7 katika mpango wa mapendekezo ya kuwa na timu 48 wakati wa fainali za kombe la dunia.

Matangazo ya kibiashara

Infantino alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Accra, Ghana ambako amefanya ziara ya siku moja na kusema kuwa "Afrika itakuwa na uwakilishi wa zaidi ya timu 7, na sasa idadi kamili inafanyiwa kazi," alisema kinara huyo wa fifa.

Kiongozi huyo amethibitisha pia, ufadhili wa maendeleo wa soka kwa bara la Afika kutoka fifa umeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 27 hadi dola milioni 94 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya kuongeza maendeleo zaidi.

Wakuu wa mashirikisho ya soka barani Afrika hivi karibuni walidokeza kutaka kupewa nafasi 10 katika nyongeza ya timu kwenye fainali za kombe la dunia zijazo, idadi ambayo ina maanisha wanataka idadi mara mbili ya sasa.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino. REUTERS/Naseem Zeitoon

Ombi hii la viongozi wa mashirikisho barani Afrika, lilitolewa wakati wa mkutano wa siku mbili uliofanyika nchini Afrika Kusini wiki iliyopita.

Kumekuwa na taarifa kuwa, nyongeza ya timu 48 kwenye michuano ijayo inalenga kulipa bara la Afrika nafasi 9, mpango ambao unatarajiwa kuanza kutumiwa kwenye fainali za mwaka 2026.

Bara la Afrika limekuwa na nafasi 5 toka kwenye fainali za mwaka 1998 nchini Ufaransa, lakini hadi sasa hakuna timu yoyote kutoka Afrika iliyowahi kushinda taji hilo.

Bara la Ulaya pia linalenga kuomba kupewa nafasi na kufikia timu 16 kutoka 13, Asia inataka kuwa na timu 8 hadi 9 kutoka timu 4 na bara la America linataka timu 6 kutoka timu 4.

Maamuzi ya mwisho kuhusu namna mgawanyo wa nyongeza wa timu utakavyokuwa utatolewa wakati wa mkutano wa baraza kuu la fifa, idadi ya wajumbe kutoka Afrika kwenye baraza la fifa, pia imeongezeka kutoka uwakilishi wa watu wa nne hadi kufikia saba.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.