UGANDA

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Uganda azuiwa kurudi nchini mwake

Kiongozi Mkuu wa Upinzani Nchini Uganda Kizza Besigye akiwa chini ya ulinzi wa polisi
Kiongozi Mkuu wa Upinzani Nchini Uganda Kizza Besigye akiwa chini ya ulinzi wa polisi REUTERS/James Akena

Serikali ya Uganda imemzuia Kiongozi Mkuu wa Upinzani Dokta Kizza Besigye kurejea nchini humo akitokea nchi jirani ya Kenya ambako alikwenda kupatiwa matibabu ikiwa ni siku moja kabla ya kuapishwa kwa Rais Yoweri Kaguta Museveni kuongoza taifa hilo kwa ngwe nyingine.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ambayo imetolewa na Chama chake imethibitisha kuzuiwa kwa Dokta Besigye ambaye alikuwa ni miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye Shirika la Ndege la Kenya iliyokuwa inastahili kutua nchini Uganda.

Anne Mugisha ambaye ni mmoja wa Maofisa wa Juu wa Chaka cha Dokta Besigye amenukuliwa akisema Vyombo vya Ulinzi zilituma taarifa kwa Shirika la Ndege la Kenya kuwa ndege yao haitoruhusiwa kutua iwapo itakuwa mmemchukua Kiongozi huyo wa Upinzani.

Taarifa kutoka Uwanja wa Ndege wa Nairobi Joko Kenyatta zimethibitisha wamepata vitisho vya ndege yao kuzuiliwa kutua katika ardhi ya Uganda iwapo Dokta Besigye atakuwa ni miongoni mwa abiria.

Dokta Besigye ambaye alikamatwa majuma mawili yaliyopita akituhumiwa kufanya maandamano haramu ambayo yalikuwa na lengo la kushinikiza serikali kupunguza kupanda kwa gharama za maisha katika taifa hilo.

Kwenye ghasia hizo za Kampala watu wanaokadiriwa kufikia watano walipoteza maisha huku wengine mamia wakijeruhiwa na polisi ikiwashikiliwa wengine ambao walishirikia maandamano hayo.

Dokta Besigye alikuwa nchini Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya macho baada ya kupulizia gesi ya kutoa machozi na askari waliokuwa wanazima maandamano hayo.

Naye Makamu wa Rais wa Chama Cha FDC Salaamu Musumba amesema wamemshauri Dokta Besigye kutumia ndege nyingine badala ile ya awali aliyokuwa anataka kuitumia.

Wananchi wa Uganda kesho wanatarajiwa kushuhudia Rais Yoweri Kaguta Museveni akila kiapo cha kuongoza taifa hilo kwa kipindi kingine baada ya kushinda uchaguzi uliofanyika mapema mwaka huu huku hali ya usalama nayo ikizidi kuimarishwa.