LIBYA-MAREKANI

Marekani yakataa kuitambua tume ya mpito ya Libya kama serikali halali

Mmoja wa wanajeshi wa jeshi la waasi nchini Libya
Mmoja wa wanajeshi wa jeshi la waasi nchini Libya © REUTERS

Serikali ya Marekani imekataa kuitambua tume ya taifa ya mpito nchini Libya kama serikali halali licha ya viongozi wake kukutana na maofisa wa ikulu ya Marekani siku ya ijumaa akiwemo mshauri wa masuala ya usalama Ton Danilon.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa tume hiyo Mahmoud Jibril akiongozana na viongozi wengine wa juu toka tume hiyo walikutana na viongozi wa Marekani kwa mazungumzo yaliyolenga kutaka kuishawsihi nchi hiyo kuiunga mkono tume yao na kuitambua kama serikali halali ya taifa la Libya.

Hata hivyo ikulu ya Marekani baadae ilitoa taarifa kuhusiana na kile ambacho viongozi hao walizungumza na kuweka msimamo wake kuwa hawaitambui tume hiyo kama serikali halali badala yake wanafahamu kuwa inajukumu la kulinda usalama wa raia na kuhakikisha kunapatikana serikali ya kidemokrasia.

Katika taarifa hiyo imeongeza kuwa wataendelea kuwasaidia waasi hao katika kupambana na vikosi vya serikali ambavyo vimekuwa vikiwashambulia waasi hao katika miji kadhaa na kuwataka viongozi hao kuhakikisha kunapatikana serikali ya kidemokrasia itakayochaguliwa na wananchi.

Hatua ya Marekani kutoitambua tume hiyo kama utawala halali wa Libya pia imeungwa mkono na Uingereza ambayo pia waziri mkuu David Cameroon mara baada ya kukutana na viongozi wa tume hiyo alikataa kuitambua kama serikali halali ya Libya.

Viongozi wa tume hiyo wamekuwa katika ziara barani ulaya kujaribu kuzishawishi nchi ambazo zina majeshi yake katika vikosi vya NATO nchini humo kutaka kuwaunga mkono waasi hao na kuutambua uongozi wao kama utawala halali wa nchi hiyo.

Wakati huohuo kiongozi wa Libya Kanali Moamer Kadafi amjitokeza kwenye televisheni ya taifa ya nchi hiyo na kushutumu mashambulizi ya vikosi vya NATO inayoyafanya katika mji wa Tripoli na kuongeza kuwa lengo lao la kutaka kumuua halitafanikiwa.