SUDAN

Wanajeshi wa Sudan ya kaskazini walitwaa jimbo la Abyei

Ramani inayoonyesha eneo la Abyei
Ramani inayoonyesha eneo la Abyei Latifa Mouaoued/RFI

Vikosi vya majeshi ya Sudan kaskazini hatimaye vimelitwaa jimbo lenye utajiri wa mafuta la Abyei linalogombaniwa kati yake na Sudan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Maofisa wa umoja wa mataifa walioko nchini Sudan wamesema kuwa wameshuhudia maelfu ya wanajeshi wa Sudan kaskazini katika mji wa Abyei wakirandaranda huku pia kukisikika milio ya risasi katika baadhi ya maeneo ya mji huo.

Uvamizi huo wa vikosi vya Sudan kaskazini umefanyika wakati ambapo ujumbe maalumu toka baraza la usalama la umoja wa mataifa umeanza ziara nchini humo ambapo unatarajia kukutana na viongozi wa pande zote mbili ambao wanagombea eneo la mpaka wa mji huo wenye utajiri wa mafuta.

Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini amesema kuwa usiku kucha kulisikika milio ya risasi ambapo majeshi ya Sudan Kaskazini walikuwa wakitumia ndege za kivita kufanya mashambulizi na kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Sudan Kusini.

Katika upande mwingine serikali ya marekani imelaani uvamizi huo na kuvitaka vikosi vya sudan ya kaskazini kuondoka katika eneo hilo ikitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya vikosi hivyo kayika jimbo hilo.