Tripoli, Libya

NATO yafanya mashambulizi mazito Libya

Reuters

Ndege za majeshi ya jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi, NATO zimefanya mashambulizi mapya mfululizo katika mji mkuu wa nchi ya Libya, Tripoli ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za kumshinikiza kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi kuondoka madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi hayo ya anga yanadaiwa kuwa makubwa kuliko yote tangu kuanza kwa operesheni hiyo ya kijeshi nchini Libya.

Mashambulizi yalilenga maeneo mbalimbali yakiwemo makazi ya Gaddafi ya Bab Al-Aziziya hatua ambayo inaelezewa kuwa itaendelea kudhoofisha nguvu za kijeshi za Gaddafi.

Mashambulizi hayo yamekuja baada ya Ufaransa kutamka kuwa itafanya mashambulizi na Uingereza kuunga mkono hatua hiyo kwa kurusha helkopta za kijeshi.

Majeshi ya NATO yako nchini Libya kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa, UN la kulinda raia wa nchi hiyo na wachambizi wa mambo wanadai NATO inakiuka azimio hilo kwa kufanya mashambulizi ambayo yanawaathiri raia badala ya kuwalinda.