SUDAN - UN

Serikali ya Sudan Kaskazini yaendelea kukaidi azimio la Umoja wa mataifa UN

Picha ikionyesha eneo la mji wa Abyei
Picha ikionyesha eneo la mji wa Abyei (Photo: Reuters)

Serikali ya Sudan Kaskazini imeendelea kukaidi agizo la baraza la usalama la umoja wa mataifa linaloitaka nchi hiyo kuondoa vikosi vyake katika jimbo la Abyei.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa habari nchini humo Rabie Abdelati amesema kuwa nchi yake haitaviondoa vikosi vyake katika jimbo hilo kwa shinikizo toka umoja wa mataifa bali mzozo huo utatatuliwa na serikali mbili yani sudan kusini na kaskazini.

Siku ya ijumaa baraza la usalama kwa kauli moja lilipitisha azimio linaloitaka serikali ya Sudan Kaskazini kuondoa vikosi vyake vilivyoko katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Abyei.

Tangazo hilo la serikali ya sudan Kasakazi linatolewa ikiwa zimepita saa chache tangu baraza la usalama la umoja wa mataifa lifikie maazimio ya kuitaka ncho hiyo kuondoa vikosi vyake katika jimbo la abyei lenye utajiri wa mafuta na linalogombewa na nchi hizo mbili.

Majeshi ya Sudan Kaskazini yamelitwaa jimbo la Abyei huku zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Sudan Kusini kutangazwa kama taifa huru, hatua inayosubiriwa kwa shauku kubwa kuona namna gani mgogoro huo utakavyotatuliwa kuhusu mmiliki halali wa jimbo hilo.

Hivi karibuni rais wa Sudan Kusini Salva Kiiri alionyesha masikitiko yake kutokana na vikosi vya sudan kaskazini kuutwaa mji huo ambao sudan Kusini inadai eneo hilo ni himaya yake.

Wakati huohuo taarifa zinasema kuwa wanajeshi wa sudana kaskazini wameendelea kutwaa miji zaidi katika jimbo hilo na kuendelea kuzua hofu ya kuzuka kwa machafuko zaidi.