MISRI

Upinzani waungana nchini Misri

Kiongozi wa chama cha Muslim Brotherhood cha nchini Misri Mohamed Badie
Kiongozi wa chama cha Muslim Brotherhood cha nchini Misri Mohamed Badie Reuters

Chama kikuu cha upinzani nchini Misri cha Muslim Brotherhood kimeunganisha nguvu na vyama vingine vya upinzani wakati huu ambapo nchi hiyo inajiandaa kuelekea uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika mwezi wa tisa mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa, viongozi wa vyama vya Muslim Brotherhood, Justice The liberal Wafd na Noor walifanya mkutano siku ya jumanne na kukubalina kuungana kwaajili ya kusimamisha wagombea toka vyama hivyo katika uchaguzi huo.

Msemaji wa chama cha Muslim Brotherhood amesema kuwa chama chake kimeamua kuunganisha nguvu na vyama vingine vya upinzani kwa lengo la kutaka kupata viti vingi zaidi katika uchaguzi ujao.

Serikali ya kijeshi ambayo inaongoza nchi hiyo ilitangaza miezi kadhaa iliyopita kuwa uchaguzi mkuu wa wabunge utafanyika mwezi wa tisa mwaka huu na kuvitaka vyama vya siasa nchini humo kujiandaa na uchaguzi huo.

Wakati huu ambapo vyama vya siasa vya zamani na vile vipya nchini humo vikiendelea kujiandaa, kumekuwa na miito mbalimbali toka kwa wanaharakati nchini humo wakitaka uchaguzi huo usogezwe mbele.

Juma lililopita waziri mkuu Essam Sharaf aligusia kuhusu uwezekano wa uchaguzi huo kusogezwa mbele na kuongeza kuwa watakaa na viongozi wa vyama vya siasa kujadili swala hilo.

Wakati wa utawala wa rais Hosni Mubarak, chama kikuu cha upinzani cha Muslim Brotherhood kilipigwa marufuku kufanya kazi zake nchini humo kwa kile kilichodaiwa kuwa mrengo wake ulikuwa unachochea vurugu nchini humo.

Hata hivyo mara baada ya kuangushwa kwa utawala wa Mubarak, chama hicho klisajiliwa tena na kuanza kutekeleza kazi zake huku chama tawala cha Rais Mubark kikifutwa rasmi kama chama cha siasa nchini humo.