Senegal-Dakar

Hali ya wasiwasi yazuka nchini Sénégal kutokana na rasimu ya sheria ya uchaguzi

Moja mwa kata za mji mkuu wa Sénégal-Dakar
Moja mwa kata za mji mkuu wa Sénégal-Dakar © (CC)/Mostroneddo

Kambi ya wapinzani nchini Senegal, imeitisha maandamano makubwa dhidi ya rasimu ya sheria ya uchaguzi, wanayoamini kuwa ni njama tu za Rais Abdoulaye Wade, kumrithisha uongozi mwanae Karim Wade hapo mwakani.

Matangazo ya kibiashara

Hayo yanatukia wakati bunge likitarajiwa kujadili mapendekezo hayo, ambayo yataongeza nafasi ya makamu wa rais, katika kinyang'anyiro cha urais, miezi minane ijayo.

Rasimu hiyo inafuta asilimia 51 ya kura zinazompa ushindi mgombea katika duru ya kwanza, na iwapo itapita mgombea atahitaji asilimia 25 tu, na kama vile haitoshi, makamu wa rais ataingia madarakani, bila kupingwa.

Huko mjini Kaolack, kilomita mia mbili hivi kutoka mji mkuu Dakar, polisi wamewarushia moshi wa machozi wapinzani waliokuwa wakiandamana jana, kupinga mapendekezo ya mabadiliko ya katiba.

Na mjini Pikine, vijana waliweka vizuizi na kuchoma moto matairi kabla ya askari wa kutuliza ghasia kuingilia kati na kuwakamata.