Nigeria-Maiduguri

Watu zaidi ya 100 wakamatwa nchini Nigeria kwa kutuhumiwa kuhusika na mashambulizi

Kituo mojawapo cha polisi mjini Maiduguri
Kituo mojawapo cha polisi mjini Maiduguri AFP/Pius Utomi Ekepei

Polisi nchini Nigeria imesema kuwa imefanikiwa kuwakamata watu zaidi ya 100 ambao wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya mabomu katika mji wa Maiduguri.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa kikosi maalumu cha polisi kinachosimamia zoezi hilo, Marilyn Ogar amesema kuwa msako wa kuwakamata watu hao ulifanywa katika maeneo mbalimbali ya kaskazini mwa nchi hiyo ikiwemo katika miji ya Kano, Adamawa, Maiduguri, Kaduna na Borno miji ambayo inasadikika kuwa na wafuasi wengi wa kundi la Boko Haram.

Aidha polisi wameongeza kuwa wanaendelea na msako katika maeneo mengine ambayo wamepokea taarifa ya kuwepo kwa wafuasi hao huku wakikataa kutaja majina ya watu ambao wamekamatwa mpaka sasa kwa sababu za kiusalama.

Maeneo ya kaskazini mwa nchi ya Nigeria yamekuwa katika hali tete kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu yanayotuhumiwa kufanywa na kundi moja la waislamu lenye uhusiano na Boko Haram.