Malawi-Uingereza

Upinzani nchini Malawi wamtwika lawama Raisi wa nchi hiyo kukwamisha msaada wa Uingereza

Kufuatia hatua ya nchi ya Uingereza kutangaza kutotoa msaada wa fedha kusaidia bajeti ya nchi ya Malawi, upinzani nchini humo umemtupia lawama rais Bingu wa Mutharika kuifikisha nchi hiyo hapo ilipo.

Bingu Wa Mutharikia, rais wa Malawi
Bingu Wa Mutharikia, rais wa Malawi Word Ecomic Forum
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa chama cha Malawi Congress Party, Nancy Tembo amesema kuwa serikali ilifanya maamuzi yenye hasira kuvunja uhusiano wa kibalozi na nchi ya Uingereza wakati akijua fika nchi hiyo inategemea kwa kiasi kikubwa msaada wa nchi hiyo.

Miezi michache iliyopita rais Mutharika alitangaza kusitisha uhusiano wa kibalozi na nchi ya uingereza kufuatia matamshi ya balozi wake nchini humo ya kukosoa utendaji wa serikali yake.

Siku ya alhamisi msemaji wa mfuko wa kuchangia maendeleo wa serikali ya Uingereza alitangaza mfuko huo kusitisha msaada wa kifedha wa zaidi ya euro milioni 19 kwenye bajeti ya serikali ya malawi kwa kile kilichotokea.

Wabunge wa upinzani nchini humo wameishutumu serikali yao wakitaka iombe radhi kwa nchi ya uingereza ili kuweza kupatiwa fedha hizo ambazo nchi ya uingereza ndio mshirika mkubwa wa bajeti ya nchi hiyo.