Misri

Wananchi wa Misri wajitokeza kwa wingi katika maandamano mjini Cairo

Eneo la Tahrir
Eneo la Tahrir Reuters / Asmaa Waguih

Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika uwanja wa Tahriri mjini Cairo Misri katika maandamano yanayolenga kuongeza shinikizo la kujiuzulu kwa serikali ya mpito ya kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati na vyama vya upinzani walioitisha maandamano hayo wamesema kuwa wamechoshwa na utawala huo ambao wamedai unatumia mabavu pamoja na kuchelewa kuchukua maamuzi katika mambo ambayo walikubalina awali.

Maandamano hayo yanakuja wakati ambapo juma hili waziri mkuu wa Misri Essam Sharaf alimuagiza waziri wake wa mambo ya ndani Mansur Essawy kuwaachisha kazi maofisa wote wa serikali waliohusika na mauaji ya raia wakati wa utawala wa Hosni Mubarak.

Tayari amri ya waziri mkuu Sharaf imefanyiwa kazi ambapo zaidi ya askari 600 wametangazwa kufutwa kazi katika hatua inayolenga kutekeleza matakwa ya waandamanji hao wanaotaka mabadiliko katika jeshi na polisi nchini humo.