MISRI

Hali ya kiafya ya rais wa zamani wa Misri yaendelea kuzorota

Hosni Mubarak
Hosni Mubarak Reuters

Hali ya kiafya ya aliyekuwa rais wa Misri Hosni Mubarak, imeelezwa kudhoofika na kuwa hivi sasa kiongozi huyo anapata ugumu wa kula chakula kutokana na hali yake kuzorota.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa iliyotolewa na afisa mmoja wa serikali ya Misri, amesema kuwa mbali na kusumbuliwa na matatizo ya saratani kiongozi huyo pia anakabiliwa na msongo wa mawazo.

Kufuatia kutolewa kwa taarifa hiyo wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani wameonekana kupinga taarifa hiyo wakitaka kiongozi huyo kupandishwa kizimbani juma lijalo kujibu mashtaka yanayomkabili.

Mwendesha mashtaka wa serikali, amesema kuwa ofisi yake inatarajia kumpandisha kizimbani kiongozi huyo juma lijalo kujibu mashtaka yanayomkabili baada ya kukamilika kwa uchunguzi kuhusiana na tuhuma za rushwa zinazomkabili kiongozi huyo.

Mubarak anakabiliwa na mashtaka ya Rushwa, mauaji ya watu na kutumia mabavu kuitawala nchi hiyo.

Serikali ya mpito nchini Misri imeanza kuwafikisha mahakamani viongozi waliokuwa chini ya utawala wa Hosni Mubarak ambapo tayari viongozi kadhaa wamekwisha hukumiwa.