AFRIKA KUSINI

Hatma ya kiongozi wa Umoja wa Vijana wa ANC Julius Malema kujulikana hii leo

Kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini, Julius Malema
Kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini, Julius Malema Reuters/Siphiwe Sibeko

Wakati kamati kuu ya chama tawala cha Afrika Kusini cha African National Congress ANC wakikutana hii leo mjini Johanesberg kumjadili kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho Julius Malema, polisi wamekabilina na wafuasi wa kiongozi huyo.

Matangazo ya kibiashara

Polisi nchini humo wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya maelfu ya vijana ambao wanamuunga mkono Malema wakipinga kile ambacho kinataka kuamuliwa na kamati ya juu ya chama hicho.

Vijana hao ambao wamejitokeza wakiwa na Fulana zenye picha ya Malema na maandishi ya kukejeli uongozi wa rais Jackob Zuma, wamemshutumu vikali rais Zuma kwa kutaka kummaliza kisiasa Malema.

Malema mwenyewe amesema yuko tayari kwa maamuzi yoyote ambayo yataamuliwa na kamati kuu na kuongeza kuwa msimamo wake unabakia palepale kuhusu siasa za Botswana.

Kamati hiyo inakutana hii leo kujadili matamshi na mwenendo wa kiongozi huyo wa Umoja wa Vijana aliyetangaza hadharani kutaka kuipindua serikali ya Botswana kwa kile alichodai ni ukosefu wa Demokrasia nchini humo.