NIGERIA

Mafuriko nchini Nigeria yasababisha vifo vya watu 102

Moja ya mafuriko yaliyoikumba nchi ya Nigeria mwaka jana
Moja ya mafuriko yaliyoikumba nchi ya Nigeria mwaka jana Online

Watu wanaokadiriwa kufikia mia moja na mbili wamepoteza maisha hadi sasa baada ya mafuriko yaliyoambatana na mvua kali kuchangia kuvunjika kwa kuta za Bwawa la Eleyele sambamba na madaraja mengine kadhaa kuharibiwa vibaya.

Matangazo ya kibiashara

Takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Nigeria kupitia Mratibu wa Majanga Umar Mairiga amethibitisha idadi ya vifo kuongezeka baada ya taarifa za hapo awali kuonesha idadi ikiwa ni ndogo.

Madaraja kadhaa yamevunjika baada ya kushuhudiwa kwa mvua kali iliyopiga kwa kipindi cha saa saba kwenye Mji wa Chuo Kikuu cha Ibadan uliopo kilometa 150 Kaskazini mwa Mji wa Lagos.

Mairiga amesema hadi sasa wamezihifadhi zaidi ya familia themanini katika majengo ya shule yamsingi ili kuweza kuwapatia malazi na chakula katika kipindi hiki ambacho wamekumbwa na matatizo ya mafuriko.

Taarifa hiyo ya Mairiga imeongeza kuwa Wilaya saba kati ya nane katika Mji wa Ibadan zimeathirika vibaya na mafuriko hayo ambayo yamekuwa yakitokea kila mara wakati wa msimu wa mvua.

Tayari Kitnego cha Maafa nchini Nigeria kimeanza kusambaza chakula, magodoro na blanketi kwa waathirika wa mafuriko hayo ambayo yanatajwa kuwa mabaya zaidi katika kipindi cha hivi karibuni.

Mwezi Julai mwaka huu mafuriko kama hayo yalitokea katika mji wa Lagos na kusababisha watu zaidi ya ishirini kupoteza maisha wakati hapo awali mwezi Juni watu ishirini na wanne walipoteza maisha baada ya mvua kali kunyesha.

Kipindi cha mwezi April hadi Septemba ya kila mwaka nchi ya Nigeria imekuwa ikikumbana na misukosuko ya kukabiliwa na mafuriko kutokana na kipindi hicho kuwa cha msimu wa mvua za masika.

Mapema mwaka jana nchi ya Nigeria ilishuhudia jirani zake Benin ikikumbana na mafuriko mabaya ambapo zaidi ya watu elfu hamsini na tano walipoteza makazi na wengine elfu sitini na nane wakiathirika.