RWANDA

Kesi ya Kiongozi wa Upinzani nchini Rwanda Victorie Ingabire kuanza kesho

Julian Rubavu

Kesi inayomkabili Kiongozi wa Upinzani nchini Rwanda kutoka Chama Cha UDF Victoire Ingabire Umuhoza ambaye anatuhumu kutishia Usalama wa Taifa hilo inatarajiwa kuanza kusikilizwa hiyo kesho.

Matangazo ya kibiashara

Kesi ambayo imeshaahirishwa mara mbili hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa mawakili wa Ingabire inatarajiwa kuanza baada ya mawakili wake kusema wapo tayari kujitokeza mahakamani kwa ajili ya kuanza utetezi.

Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa tarehe 16 ya mwezi May lakini ikaahirishwa na hata mara ya pili ambapo ilitakiwa kuanza tarehe 20 ya mwezi June ilishindikana tena.

Mawikili wa upande wa utetezi walihitaji muda zaidi kupitia nyaraka zenye kurasa 2500 ambazo zilihitajika kuyafsiriwa na mawakili hao ili kujua namna ambavyo wanaweza kuanza kibarua chao cha kumtetea mteja wao.

Mwanasheria wa Ingabire, Gatera Gashabana amesema kwa sasa wapo tayari kuanza utetezi dhidi ya mteja wao ambaye amekuwa akipewa mashtaka kutokana na sababu za kisiasa ili asiwe na uwezo kuleta upinzani kwa serikali.

Mwanasheria Gashabana amesema tafsiri zote ambazo zilikuwa zinahitajika zimeshafanywa na wanauhakika wa kupangua mashtaka yote ambayo yanamkabili mteja wao licha ya serikali kukanusha uwepo wa uhusiano wa kisiasa na kesi hiyo.

Mashtaka ambayo anatuhumiwa kuyafanya Ingabire ni pamoja na kutajwa kufadhili makundi ya kigaidi likiwemo la FDLR lakini Mwanasheria wake Gashabana amesema hiyo yote ni kutokana na nguvu ambavyo mteja wao kwenye siasa.

Victoire Ingabire Umuhoza alirejea nchini Rwanda mnamo mwezi January mwaka 2010 baada ya kuishi uhamisho Uholanzi kwa kipindi cha miaka 17 na anashikiliwa gerezani tangu tarehe 14 ya mwezi Oktoba mwaka 2010.