Libya

Kiongozi wa NTC auhutubia umma kwa mara ya kwanza jijini Tripoli

Waasi wa Libya wakilinda usalama wakati kiongozi wao akihutubia umma Septemba 12,2011.
Waasi wa Libya wakilinda usalama wakati kiongozi wao akihutubia umma Septemba 12,2011. REUTERS/Suhaib Salem

Kiongozi wa baraza la mpito nchini Libya Moustapha Abdeljalil amewahutubia maelfu ya wafuasi wake jijini Tripoli ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu walipofaulu kumfurusha kanali Gaddafi na wafuasi wake jijini Tripoli. Kiongozi huyo alipokelewa kwa shangwe wakati alipo simama kuwahutubia wananchi waliokuja kusikiliza hotub yake.

Matangazo ya kibiashara

Akiwahutubia wananchi hao, kiongozi wa baraza la mpito ameuambia umati huo misimamo ya wastani ya Kiislamu ndio itakayokuwa kiini cha sheria za taifa jipya la Libya baada ya serikali ya Gaddafi kungolewa madarakani. Amesema, hawatokubali nadharia kali za mrengo wa kulia wala wa kushoto.

Abdel-Jalil aliwasili Tripoli siku ya Jumamosi kwa mara ya kwanza tangu serikali ya Gaddafi kutimuliwa.

Kiongozi wa baraza la mpito la Libya, Mustafa Abdel Jalil alikumbusha kuwa taifa bado halijakombolewa. "Bado hatujakuwa huru, kwani Gaddafi ana fedha na dhahabu. Anaweza kuwanunua wapiganaji wepya. Tufahamu vizuri kuwa Gaddafi bado hajamalizika."

Wakati huo huo, vikosi vya Muammar Gaddafi kwa ghafula vimeshambulia upya kutoka pande tatu, huku Gaddafi akiapa kuwa ataendelea kupigana kutoka mafichoni mpaka ushindi utakapopatikana.

Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye stesheni ya televisheni ya Arrai Oruba iliyo na makao yake nchini Syria, Gaddafi amesema, haiwezekani kabisa kuitoa tena Libya kwa wakoloni.

Hapo jana, vikosi vyake vilivyobakia vilishambulia mji wa Ras Lanuf wenye kiwanda cha kusafishia mafuta, mashariki ya nchi.

Mapigano mengine yalitokea kwenye barabara inayoelekea mji wa Sirte, alikozaliwa Gaddafi na mji wa Bani Walid kusini-mashariki ya mji mkuu Tripoli. Lakini tangu vikosi vya Baraza la Mpito NTC kuuteka mji mkuu Tripoli, vikosi hivyo vimefanikiwa kusonga mbele kuelekea mji wa Sirte unaoadhibitiwa na wafuasi wa Gaddafi.