SUDANI KUSINI-MAREKANI-SUDANI

Sudani Kusini yataka mazungumzo na Jamhuri ya Sudani kumaliza tofauti zao

Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir (Kushoto) akiwa na Rais Omar Al Bashir wa Sudani
Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir (Kushoto) akiwa na Rais Omar Al Bashir wa Sudani REUTERS/Goran Tomasevic

Taifa jipya la Sudan Kusini limetaka mazungumzo ya mapatano ambayo yanatejesha uhusiano mwema baina yao na majirani zao wa Sudan ambao wamejitenga nao Rais wa nchi hiyo Salva Kiir ameuambia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambao unaendelea nchini Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Rais Kiir akihutubia Mkutano huo amesema kuwa japokuwa kuna baadhi ya mambo ambayo wanasigana na wenzao wa Sudan lakini anahitaji mazungumzo yafanyike na hatimaye mataifa hayo mawili yapatane na kuachana na migogoro ya kila kukicha inayosababisha vifo vya wananchi wasio na hatia.

Kiongozi huyo wa Sudan Kusini amewaambia wajumbe kuwa tatizo kubwa ambalo limekuwa likichangia kushindwa kufikiwa kwa muafaka na wenzao wa Sudan ni kutoafikiana juu ya mipaka ambayo inastahili kutumika.

Rais Kiir amesema wameshatoa mapendekezo yao kwa serikali ya Jamhuri ya Sudan katika kuhakikisha inashughulikia suala hilo la mipaka ambalo linachangia machafuko katika majimbo ya Abyei, Kordofan Kusini na Blue Nile.

Kiongozi huyo wa Sudan Kusini amesema kabla ya nchi hiyo haijaweza kusimama yenyewe ni lazima ihakikishe uhusiano wake na Jamhuri ya Sudan ambayo ilikuwa adui yake unaimarika haraka iwezekanavyo.

Katika hatua nyingine Rais Kiir ameomba msaada kwa mataifa kusaidia kuijenga upya nchi yake kutokana na moja ya mataifa maskini kutoka na kushuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa.

Rais huyo wa Sudan Kusini ameongeza kuwa katika mataifa yote ambayo yamepitia kwenye vita huwa yanatarajia kujengwa upya lakini hilo si suala ambalo linaweza kufanikiswa na nchi yake pekee bila ya kupata msaada.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake tarehe kenda ya mwezi Julai mwaka huu baada ya wananchi wa eneo hilo kupiga kura ya maamuzi ya kujitenga kutoka Utawala wa Sudan ambao upo chini ya Rais Omar Hassan Al Bashir.