LIBERIA

Wananchi wa Liberia wanapiga kura kuchagua Rais na Wabunge

Reuters

Wananchi wa Liberia leo wanapiga kura kuchagua rais pamoja na wabunge ukiwa ni uchaguzi wa kwanza kusimamiwa na taifa hilo baada ya kushuhudia miaka kumi na minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofikia tamati mwaka elfu mbili na tatu.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa sasa na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Ellen Johnson Sirleaf anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa Winston Tubman ambaye mgombea mwenza wake ni Mchezaji bora wa zamani wa Dunia George Weah.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi James Fromayan amesema vituo vimefunguliwa saa mbili asubuhi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wapigakura milioni moja na laki nane ambao wamejiandikisha nchini humo.

Uchaguzi huo huenda ukaingia kwenye duru la pili iwapo mshindi hatoweza kupata zaidi ya nusu ya kura zote ambazo zitapigwa na hivyo wagombea wawili wenye wingi wa kura watapambana kwenye uchaguzi mwingine wa terehe nane mwezi Novemba.

Uchaguzi huu unachukuliwa kama kipimo cha ukomavu wa demokrasia katika nchi ya Liberia kwani taifa hilo limekataa Umoja wa Mataifa UN kusimamia uchaguzi huo na badala yake kazi hiyo wataifanya wenyewe.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa tarehe ishirini na sita ya mwezi Oktoba licha ya matokeo ya awali kuanza kupatikana kwenye vituo kuanzia usiku wa leo.

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika Magharibi ECOWAS James Victor Ghebo amenukuliwa akisema kuwa maandalizi yote yamekamilika ikiwemo ni pamoja na kufika kwa waangalizi wa uchaguzi huo.

Rais wa sasa Sirleaf ambaye kampeni zake ziliongezwa nguvu na ushindi wake wa Tuzo ya Amani ya Nobel anatarajiwa kuwa na wakati mgumu katika harakati zake za kuomba ridhaa ya kuongoza kwa miaka sita mingine licha ya kufanikiwa kurejesha ustawi katika nchi hiyo.

Liberia ni moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na umaskini mkubwa wa wananchi wake kitu ambacho Rais Sirleaf ameendelea kutumia katika kuomba kura akijinadi kuna masuala ambayo anahitaji kuyamalizia ili maisha ya wananchi yaweze kuwa bora.

Wananchi wa Taifa hilo na dunia kwa pamoja wanakumbukumbu nzuri ya maneno ya Rais Sirleaf ambaye alisema anataka kuongoza nchi hiyo kwa kipindi kimoja lakini sasa imekuwa tofauti na anawania ngwe ya pili.