CAMEROON

Upinzani Cameroon wataka matokeo yabatilishwe.

Rais wa Cameroon Paul Biya ambaye anawania kuchaguliwa kwa mara nyingine.
Rais wa Cameroon Paul Biya ambaye anawania kuchaguliwa kwa mara nyingine. REUTERS/Akintunde Akinleye

Wakati matokeo ya Urais nchini Cameroon yakiendelea kusubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi wa taifa hilo, upinzani unataka matokeo ya mwisho yatakayotangazwa yabadilishwe.

Matangazo ya kibiashara

Ni zoezi la uhesabuji kura ambalo hii leo limeingia siku yake ya tatu toka upigaji kura ulipofanyika ambapo mpaka sasa tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo haijafanikiwa kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi huo.

Siku ya jumanne upinzani nchini cameroon ulitaka matokeo ya uchaguzi huo yabatilishwe na uchaguzi kurejewa upya kwa kile walichodai kuwa haukuwa huru na haki na kulikuwa na kila njama za kutaka kukipendelea chama tawala ili kiibuke na ushindi.

Akizungumza na waandishi wa habari kiongozi wa upinzani John Fru Ndi ambaye amegombea nafasi hiyo kwa mara ya nne mfululizo ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuchelewa kutangazwa kwa matokeo na kuongeza kuwa hizi ni njama za rais Paul Biya kutaka kupewa ushindi.

Licha ya malalamiko ya Upinzani, rais Biya mwenye ameonekana kuwa mtu mwenye matumaini ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo huku akisisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki na hakuna cha kurudia kuhesabu.

Bado tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo haijatangaza ni wakati gani hasa matokeo rasmi yatatangazwa.