TUNISIA

Matokeo rasmi ya Uchaguzi wa Wabunge nchini Tunisia kutangazwa jumanne

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tunisia inatarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi wa wabunge ambao umefanyika jana hiyo kesho baada ya hii leo kuanza kutolewa matokeo ya awali ya majimbo kadhaa. 

. REUTERS/Zoubeir Souissi
Matangazo ya kibiashara

Wananchi wa Tunisia na Dunia kwa ujumla wanaendelea kusubiri kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa kwanza kidemokrasia kufanyika nchini Tunsia tangu nchi hiyo ipate uhuru wake zaidi ya miaka hamsini iliyopita.

Uchaguzi huu umekuja ikiwa ni miezi tisa tangu kuangushwa kwa utawala wa Rais wa zamani Zine El Abidine Ben Ali ambaye aliondolewa madarakani kwa nguvu ya umma baada ya wananchi wa taifa hilo kuchoshwa na hali ngumu ya maisha.

Matokeo hayo yanatarajiwa kutolewa hii leo baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza mapema kuwa matokeo ya uchaguzi huo wa kwanza wa wabunge yatatangazwa saa kumi na nne baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.

Uchaguzi huo ndiyo utaamua kina nani ambao wanastahili kuwa wabunge wapya katika Bunge la nchi hiyo ambalo linakuwa na wawakilishi mia mbili kumi na saba kutoka katika kila kona ya taifa hilo.

Chama cha Kiislam cha Ennahda ndicho ambacho kinapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa wingi wa viti katika uchaguzi huo kutokana na kuungwa mkono na wananchi wengi kutokana na sera walizonazo.

Wananchi wa taifa hilo wakiwa wanasubiri matokeo ya uchaguzi wamesema baada ya uvumilivu wa miongo zaidi ya mitano hatimaye wamefanikiwa kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua wabunge wanaowataka.

Uchaguzi huo umepongezwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ambaye amesema kuendeshwa kwa zoezi hilo kwa amani na utulivu kunadhihirisha mwanzo wa demokrasia kwenye nchi hiyo.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama Cha Kiislam cha Ennahda Rached Ghannouchi ameonekana ni mwenye furaha huku akisema wanauhakika wa kupata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo.

Wananchi wa Tunisia walifanikiwa kuuangusha utawala uliodumu kwa kipindi cha miaka ishirini na mitatu madarakani chini ya Rais Ben Ali mapinduzi ambayo yalifuata katika nchi za Misri na baadaye Libya.