KENYA-SOMALIA

Majeshi ya Kenya kuondoka Somalia wakiwasambaratisha Wanamgambo wa Al Shabab

Serikali ya Kenya imeahidi majeshi yake pamoja na vifaru ambavyo wamevipeleka Kusini mwa Nchi ya Somalia yataondolewa huko mara tu watakapokuwa wamefanikiwa kulisambaratisha Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab lenye uhusiano na Mtandao wa Al Qaeda.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Serikali ya Kenya Alfred Mutua amesema mkakati wa majeshi yao ni kuhakikisha wanalisambaratisha Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab lenye maskani yake nchini Somalia katika kipindi kifupi.

Mutua amewaambia wanahabari ya kwamba majeshi ya Kenya hayatakuwa tayari kuendelea kusalia nchini Somalia pale ambapo watakuwa wamemaliza mpango wao wa kulimaliza Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab.

Msemaji huyo wa serikali ya Kenya amesema kile ambacho wanakifanya ni halali kabisa kwani hata Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika IGAD na Umoja wa Afrika AU wote wamekuwa wakihimiza uwepo wa amani.

Mutua amesema serikali yake ilifanya majadiliano na Marekani, Ufaransa, Uingereza na washirika wake wengine kabla ya kuanzisha operesheni hiyo lakini hakuna majeshi mengine ambayo yameshirikishwa kwa sasa zaidi ya lile la Kenya.

Mutua ameweka bayana wakishahakikisha wamemaliza jukumu la kulisambaratisha Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab watarejesha jukumu la kulinda amani kwa Majeshi ya Umoja wa Afrika AU yaliyopo nchini Somalia.

Opereshani ya Linda Nchi Dhidi ya Al Shabab imeingia siku ya kumi na mbili lakini tayari ilishakosolewa na Rais wa Somalia Sheikh Sharif Ahmed ambaye amesema majeshi ya Kenya yamevamia nchi yake bila ya ruhusa yao.

Rais Ahmed ameongeza kuwa hawapo radhi na hatua ya majeshi ya Kenya kuingia katika ardhi yao bila ya kupata ruhusa ya kuendesha operesheni yao ya kuwasaka wanamgambo wa Al Shabab.

Katika hatua nyingine watu wanne raia wa Kenya wamepoteza maisha kwenye eneo la mpaka wa nchi yao na Somalia baada ya kutekelezwa kwa shambulizi la tatu katika kipindi cha juma moja tangu majeshi yake yaingie kuwaska Al Shabab.

Taarifa zinaeleza kuwa watu wanane wakiwa wamejihami kwa maguruneti na bunduki za kivta walivamia eneo la Mandera na kushambulia kisha wakatoweka kusikojulikana na hawajabainika ni kina nani.