MONROVIA-LIBERIA

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Liberia ajiuzulu wadhifa wake

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Nchini Liberia James Fromayan amejiuzulu wadhifa wake wakati nchi hiyo inaeleka kwenye duru la pili la uchaguzi wa Rais ambao utafanyika tarehe nane ya mwezi Novemba.

Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Liberia (katikati) aliyejiuzulu, James Fromayah
Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Liberia (katikati) aliyejiuzulu, James Fromayah REUTERS/Luc Gnago
Matangazo ya kibiashara

Fromayan amefikia uamuzi wa kujiuzulu baada ya upinzani nchini Liberia kumtuhumu kuhusika kwenye wizi wa kura kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi ambacho kilifanyika tarehe kumi na moja oktoba ambapo mshidni hakupatikana.

Kiongozi Mkuu wa Upinzani Winston Tubman ambaye alipata asilimi thelathini na mbili nukta saba ya kura zote alishusha tuhuma nzito ya kwamba kulikuwa na ulaghai mwingi kwenye matokeo ambayo yalimpa uongozi Rais Ellen Johnson Sirleaf ambaye alipata asilimia arobaini na tatu nukta kenda.

Awali kambi ya upinzani nchini humo ilitishia kutoshiriki katika duru la pili la uchaguzi huo endapo mwenyekiti huyo asingejiuzulu nafasi yake wakimtuhumu kuwa alichangia pakubwa upinzani kushindwa kwenye uchaguzi huo.

Rais Sirleaf mwenyewe amepuuzia mbali madai ya upinzani akiamini kuwa atasalia madarakani hata baada ya matokeo ya duru la pili kutangazwa.

Uchaguzi nchini Liberia unatazamwa kwa karibu na jumuiya ya kimataifa hasa baada ya kushuhudia nchi hiyo ikirejea katika demokrasia miaka 6 iliyopita baada ya kuwa katika vita vya muda mrefu.