KENYA-SOMALIA

Kundi la Al-Shabab nchini Somalia latishia kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya vikosi vya Kenya

Wanajeshi wa Serikali wakiwa katika moja ya mapambano na wanamgambo wa Al-Shabab mjini Mogadishu
Wanajeshi wa Serikali wakiwa katika moja ya mapambano na wanamgambo wa Al-Shabab mjini Mogadishu Reuters

Wapiganaji wa Al-shabab nchini Somalia wamesema kuwa wanaendelea kujiimarisha zaidi kujiandaa kwa vita visivyoisha dhidi ya majeshi ya Kenya ambayo yako nchini humo kuwasaka.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo imekuja Wakati vikosi vya Kenya vikijiandaa kushambulia eneo linalodhibitiwa na Al Shabaab baada ya kufanikiwa kudhibiti eneo la kusini mwa Somalia mwezi uliopita.

Taarifa ya Kundi hilo imeionya Kenya kuwa itaona madhara yake na kuwa litapambana na Kenya kama ilivyofanya kwa mataifa mengine ambayo wanadai yalijutia uamuzi wao.

Halikadhalika kundi hilo limesema kuwa lina wasiwasi kuwa kutatokea vifo vingi vya raia iwapo majeshi ya Kenya yatashambulia maeneo yao.

Awali Kenya ilitoa tahadhari kwa miji kumi ya Somalia kuondoka maeneo yanayoshikiliwa na Al Shabaab kwa kuwa inatarajia kufanya mashambulizi katika maeneo hayo.

Kenya imesema kuwa itafanya uchunguzi juu ya uwepo wa ripoti inayoeleza kuwepo kwa vifo vya raia kufuatia mashambulizi yaliyofanywa katika mji wa Jilib mwishoni mwa wiki iliyopita.