Nigeria

Watu zaidi ya sitini wauawa nchini Nigeria

Askari wa Nigeria wakiikagua gari
Askari wa Nigeria wakiikagua gari REUTERS/Afolabi Sotunde

Watu zaidi ya sitini wameripotiwa kuuawa katika shambulio kwenye mji mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria. Mashuhuda wa tukio hilo la Damaturu, mji mkuu wa jimbo la Yobe, wanasema mabomu kadha yaliripuka jana usiku na magari kadhaa yaliteketea.

Matangazo ya kibiashara

Hapo jana piya mashambulio yalifanywa na watu waliojitolea mhanga katika mji wa Maiduguri. Licha ya kwamba hakuna kundi lolote ambalo limekwisha tangaza kuhusika kwa matukio hayo, kundi la waislam wenye msimamo mkali la Boko Haram lina shukiwa kuendesha mashambulizi hayo.

Wakaazi wa Damaturu wanasema mji huo ulishambuliwa Ijumaa magharibi.
Kati ya saa kumi na mbili unusu na saa mbili mabomu yaliripuliwa katika maeneo kadha pamoja na makao makuu ya polisi katika jimbo hilo.
Risasi zilisikika hadi usiku wa manane na inaarifiwa kuwa watu wanaukimbia mji huo.

Kamishna wa polisi wa jimbo la Yobe alisema mji huo umeshtushwa na mashambulio hayo, na bado anajaribu kuchunguza watu wangapi wamekufa au kuumia.
Duru za hospitali zinaonesha kuwa watu zaidi ya sitini, wameuwa na wengine kadha kujeruhiwa.