LIBERIA-MONROVIA

Umoja wa Ulaya wasikitishwa na maamuzi ya Winston Tubman kugomea uchaguzi wa Liberia

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Liberia Winston Tubman
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Liberia Winston Tubman mamafisoa.org

Mkuu wa sera za kigeni wa EU Catherine Ashton ameonesha masikitiko yake juu ya uamuzi wa mpinzani wa nchini Liberia Winston Tubman kugomea duru la pili la uchaguzi huku Ashton akisema kuwa hatua hiyo inazorotesha demokrasia changa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Ashton amefurahishwa na matokea ya duru la kwanza la uchaguzi wa urais kwa kuwa ulikuwa wa amani na wa wazi kwa mujibu wa waangalizi wa ndani na wa nje wa uchaguzi huo.

Hata hivyo Ashton amesikitishwa na hatua ya Tubman kugomea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho na kusema kuwa hatua hii inawanyima raia wa Liberia kuchagua kiongozi wanayemtaka na hatiamae kufifisha demokrasia inayotazamiwa kujengeka.

Tubman ametoa wito kwa wapiga kura kutoshiriki zoezi la upigaji kura wa duru la pili halikadhalika amewataka wafuasi wake kufanya maandamano ya amani.

Rais wa nchi hiyo, Ellen Johnson aliyeshinda Tuzo la Amani la Nobel mwaka huu alipata asilimia 43.9 ya kura zilizopigwa katika duru la kwanza la uchaguzi akimshinda mpinzani wake Tubman aliyepata asilimia 32.7 ya kura zilizopigwa, matokeo yaliyodaiwa na upinzani kuwa ya udanganyifu.