SUDAN

Mgogoro wa Sudan wazidi kufukuta, kipindupindu chawakumba wakimbizi wa Somalia

Rais wa Sudan na Rais wa Sudan Kusini kwa pamoja wanatabiri huenda kukawepo vita nyingine ya wenyewe kwa wenyewe kama pande hizo mbili hazitafikia muafaka wa haraka katika maeneo wanayotofautiana. Kumekuwepo na taarifa kwa kuwepo kwa maandalizi ya vikosi vya majeshi ya Sudan na Sudan kusini katika mpaka huku waasi wa Sudan wakitangaza nia yao ya kuiangusha serikali yao iliyo na makao makuu yake mjini Khartoum.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Sudan Omar Al Bashir anaishutumu Sudan Kusini kwa kuyafadhili makundi ya waasi wa Sudan na kusema kuwa ikiwa Sudan Kusini inataka kurejea kwenye vita jeshi lake liko tayari na wako tayari kutoa funzo jingine kwa Sudani Kusini.

Naye Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema kuwa shutuma za Bashir ni kutafuta sababu tu ya kuvamia Sudan Kusini.

Wiki iliyopita Marekani na maafisa wengine wa kiataifa walisema kuwa ndege za majeshi ya Sudan ziliruka mpaka Sudani Kusini na kuangusha mabomu, huku shambulio jingine la bomu likifanyika dhidi ya kambi ya wakimbizi.

Katika hatua nyingine kumekuwa na taarifa kuwa watu 60 wameugua ugonjwa wa kipindupindu katika kambi ya Dadaab inayokaliwa na wakimbizi wa Somalia, huku kukiwa na taarifa kuwa mtu mmoja amepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Ofisi ya umoja wa mataifa inayoshughulikia maswala ya haki za binaadamu imesema kuwa kumi kati ya sitini walioripotiwa kuugua katika kambi ya Dadaab wamethibitishwa kwa vipimo vya maabara na mmoja akithibitishwa kupoteza maisha.

Ugonjwa huo umegunduliwa miongoni mwa wakimbizi waliowasili kutoka Somalia hivi karibuni.

Dadaab ni kambi kubwa ya wakimbizi duniani iliyo karibu na mpaka wa Kenya na Somalia,ikiwa ni makazi ya watu takriban zaidi ya laki nne.