LIBYA-TRIPOLI

Aliyekuwa mkuu wa usalama wa Taifa nchini Libya, Abdullah Al Sanussi nae akamatwa

Aliyekuwa mkuu wa Usalama wa taifa nchini Libya, Abdullah Al-Senussi
Aliyekuwa mkuu wa Usalama wa taifa nchini Libya, Abdullah Al-Senussi

Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Libya chini ya Utawala wa Marehemu Kanali Muamar Gaddafi Abdullah Al Sanussi aliyekuwa anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya ICC amekamatwa katika Mji wa Sabha serikali ya mpito imedhibitisha.

Matangazo ya kibiashara

Al Sanussi aliyekuwa Kiongozi mwandamizi kwenye serikali ya Marehemu Kanali Gaddafi alikuwa anasakwa kwa udi na uvumba amekamtwa siku moja baada ya kukamatwa kwa Saif Al Islam lakini yeye anatajwa kuwa muhimu zaidi kutokana na kuwa na siri nyingi.

Msemaji wa Serikali ya Baraza la Mpito la Taifa NTC Jalil Al Jalali amesema kukamatwa kwa Al Sanussi ambaye ni shemeji wa Marehemu Kanali Gaddafi ni kitu muhimu sana kutokana na ukaribu aliokuwa nao na ufahamu wa siri nyingi.

Hapo jana mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC Luis Moreno Ocampo amesema kuwa anajiandaa kwenda nchini Libya kwaajili ya kufanya mazungumzo na serikali ya mpito ya nchi hiyo kuangalia uwezekano wa viongozi hao kufikishwa katika mahakama hiyo.

Kumekuwa na mvutano kuhusu mahali ambako viongozi hao watashtakiwa huku baraza la mpito lenyewe likisistizia kuwa linataka watuhumiwa hao washtakiwe katika mahakama za ndani huku jumuiya ya kimataifa yenyewe ikitaka viongozi hao washtakiwe katika mahakama ya ICC.