SOMALIA

Majeshi ya Ethiopia yaingia nchini Somalia

Baadhi ya wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia
Baadhi ya wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia Reuters

Serikali ya Ethiopia imeamua kupeleka majeshi yake nchini Somalia hatua inayokuja majuma matano baada ya majeshi ya Kenya kuingia katika nchi hiyo yenye machafuko kuwasaka wanamgambo wa Al Shabab.

Matangazo ya kibiashara

Mashuhuda wamethibitisha majeshi ya Ethiopia kuingia nchini Somalia yakiwa kwenye magari ya kivita na zana kuweza kukabiliana na wanamgambo hao ili kuhakikisha nchi hiyo inaepukana na machafuko ya muda mrefu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Uamuzi wa majeshi ya Ethiopia kuingia Somalia unakuja wakati huu ambapo Umoja wa Afrika AU ukitaka Majeshi ya Kulinda Amani AMISOM yaongezewe nguvu kwa kupata askari zaidi ili kuipa nguvu serikali dhaifu ya Rais Sheikh Sharrif Ahmed.

Majeshi ya Ethiopia yameingia nchini humo kupitia upande wa magharibi mwa nchi hiyo kwa lengo la kuendelea kuwasambaratisha wapiganaji wa Al-Shabab ambao wameendelea kusalia katika miji mingi ya kusini na magharibi mwa nchi hiyo.

Nchi ya Ethiopia ilivamia nchini humo mwaka 2006 kwa usaidizi wa majeshi ya Marekani na kufanikiwa kuwasambaratisha wanamgambo hao na baadae waliviondoa vikosi vyake baada ya miaka mitatu kwa kile kilichoelezwa walishindwa kurejesha amani katika nchi hiyo.

Siku ya Ijumaa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni alipongeza hatua ya majeshi ya Ethiopia kuingia nchini humo ambapo nchi yake na Burundi ndio zenye wanajeshi wengi wakulinda amani nchini Somalia.