LIBYA-TRIPOLI

Libya kutangaza Serikali mpya hii leo

Waziri mkuu wa Libya, Abdurrahim el-Keib
Waziri mkuu wa Libya, Abdurrahim el-Keib Reuters

Waziri mkuu wa baraza la mpito nchini Libya la NTC, Abdurrahim al-Keib anatarajiwa kutangaza baraza jipya la mawaziri litakalounda Serikali mpya muda wowote kuanzia leo.

Matangazo ya kibiashara

Waziri mkuu al-Keib amesema kuwa mpaka kufikia jana jioni alikuwa anafanya marekebisho ya mwisho mwisho kabla ya kutangaza baraza hilo jipya la mawaziri linalongojewa kufahamika na jumuya ya kimataifa na wananchi wa Libya.

Akizungumza wakati wa mkutano wake na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice, waziri mkuu al-Keib ameendelea kuishukuru Serikali ya Marekani kwa mchango wake katika kuipatia ukombozi nchi yake.

Hapo jana vyombo kadhaa nchini humo vilibainisha majina ya watu ambao wanadhaniwa kuwemo kwenye baraza hilo ambapo vilimtaja kamanda aliyeongoza mapambano toka mji wa Zintan kuelekea Tripoli, Osama Al-Juwali.

Mapema hii leo kiongozi huyo anatarajiwa kuliweka wazi baraza lake la mawaziri ambalo litakuwa na jukumu la kuwaunganisha wananchi wa Libya pamoja na kuandaa mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ya nchi hiyo.