Viongozi wa vyama vitatu vya upinzani nchini Tunisia wakubaliana kugawana madaraka
Imechapishwa:
Vyama Vikuu vitatu vyenye nguvu kisiasa nchini Tunisa vimefikia makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja hatua inayokuja ikiwa ni miezi kumi baada ya kuangushwa kwa utawala wa Rais Zine El Abidine Ben Ali.
Hamadi Jebali kutoka Chama cha Ennahda ambacho kilishinda kwa wingi wa viti kwenye uchaguzi wa wabunge amekabidhiwa jukumu la kuwa Waziri Mkuu wa Nchi hiyo huku nafasi za urais na uenyekiti wa bunge zimekwenda kwa vyama vingine viwili.
Rais wa nchi hiyo sasa atakuwa Moncef Marzouki kutoka Chama Cha CPR huku Mustapha Ben Jaafar kutoka Chama Cha Ettakalo akichukua jukumu la kuongoza mkakati wa kupatikana kwa katiba mpya nchini humo.
Uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ulifanyika mwezi uliopita ambapo chama cha Ennahda kilipata ushindi na baadae vyama vingine vya upinzani kupinga ushindi wa chama hicho wakisema kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Wananchi wa Tunisia pamoja na jumuiya ya kimataifa wanasubiri kwa hamu kubwa kuona mwenendo wa Serikali itakayotangazwa na jinsi itakavyosimamia utawala wa kidemokrasia nchini humo.