LIBYA-TRIPOLI

Seif al-Islam Gaddafi kuhukumiwa na mahakama za ndani

Waziri mkuu wa Libya, Abdurrahim el-Keib
Waziri mkuu wa Libya, Abdurrahim el-Keib Reuters

Waziri mkuu mpya wa Libya Abdurrahim al-Keib ametangaza Serikali mpya ya nchi hiyo huku nafasi ya waziri wa ulinzi akimpa kamanda aliyeongoza mapambano kutoka Zintan kuingia Tripoli, Osama al-Juwali. 

Matangazo ya kibiashara

Katika baraza hilo la mawaziri pia amemjumuisha Abdurrahim Bin Yazza aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni moja ya mafuta nchini Italia kuwa waziri wa mafuta na Ashour Bin Khayal ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje.

Wengine ni waziri wa mambo ya ndani Fawzi Abdelali, Ashur bin Khayyal nayekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Hassan Zoglem anayekuwa waziri wa fedha, Issa al-Touijer anakuwa waziri wa mipango, Tahar Sharkass ameteuliwa kuwa waziri wa uchumi na Hamza Bufares anakuwa waziri wa masuala ya dini na misaada.

Mawaziri wengine katika serikali hiyo ni pamoja na Abdennasser Jibril Hamed atakayeshughulikia majanga na watu waliopotea, Mabruka al-Sherif Jibril anayekuwa waziri wa masuala ya kijamii, Suleyman Ali al-Saheli waziri wa elimu Mustafa al-Rojbani waziri wa kazi, Ali H'mida Ashur waziri wa sheria, Fatma al-Hamrush waziri wa afya.

Wengine ni Mohammed al-Hrari waziri wa serikali za mitaa, Ibrahim al-Sgutri nyumba na makazi, Yussef al-Whishi: usafiri na mawasiliano, Anwar al-Fituri: Sayansi, Suleyman Abdelhamid Bukharruba: kilimo, Mohammed Mahmoud al-Ftissi: viwanda, Naim al-Gharyani: elimu ya juu na sayansi ya utafiti, Fethi Tarbel: vijana na michezo, Abdelrahman Habil: utamaduni na Awadh Brayek Ibrahim: nishati na madini.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa Serikali hiyo mpya itakuwa na jukumu la kuhakikisha linapitia upya katiba ya nchi hiyo pamoja na kuhakiki tena wanajeshi watakaounda jeshi la Libya.

Wakati huo huo mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC Luis Moreno-Ocampo aliwasili hapo jana mjini Tripoli na kukutana na waziri wa sheria na katiba Mohammed al-Allagui na kufanya nae mazungumzo.

Wakati wa mazungumzo hayo waziri huyo wa sheria alimwambia waziwazi mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo kuwa nchi yake haitamkabidhi mtoto wa marehemu kanali Muamar Gaddafi, Seif al-Islam Gaddafi ambaye amesema atashatakiwa kwa mujibu wa sheria za Libya.

Awali kulikuwa na mtizamo tofauti kuhusu mahali ambapo mtoto huyo na aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa al-Senussi wangehukumiwa lakini sasa ni wazi kuwa viongozi hao wote wawili watashtakiwa nchini Libya.

Wanaharakati wa haki za binadamau nchini humo wameendelea na kukusanya ushahidi unaowahusisha viongozi hao na mauaji ya maelfu ya watu ambao walikufa wakati wa utawala wa serikali ya marehemu kanali Gaddafi.