GAMBIA

Jumuiya ya ECOWAS yahofia kutokea vurugu katika uchaguzi mkuu wa Gambia

Rais wa Gambia Yahya Jammeh
Rais wa Gambia Yahya Jammeh Reuters

Wananchi wa Gambia wanapiga kura ya kuchagua rais wa nchi hiyo huku kukiwa na kila dalili za rais anayetetea wadhifa wake kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi huo Yahya Jammeh kushinda kwa mara nyingine.

Matangazo ya kibiashara

Wapigakura ambao wamejiandikisha kushiriki kwenye kinyang'anyiro hicho cha uchaguzi kinachofanyika hii leo ni laki nane huku Rais Jammeh akisema ushindi wake utampa nafasi ya kuweza kumalizia kibarua cha kuwakomboa wananchi maskini.

Kabla ya kupigwa kura ya kuchagua rais nchini Gambia kumeshaibuka malalamiko ya kwamba serikali ya nchi hiyo imeshapanga njama za kuhakikisha inashinda na hivyo uchaguzi huo hautakuwa wa huru na wa haki kwa mujibu wa upinzani.

Wakati uchaguzi huo ukifanyika na kukiwepo malalamiko ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, waangalizi toka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS imekataa kupeleka wasimamizi wake baada ya kubaini kuwa tayari kumekuwa na wizi wa masanduku pamoja na karatasi za kupigia kura.

Waangalizi hao wamesema kuwa walifanya ukaguzi katika baadhi ya vituo na mwenendo wa uchaguzi huo na kubaini mapungufu mengi ambayo yanaashiria wazi kuwa chama tawala nchini humo kimepanga kuiba kura na kutaka kuendelea kusalia madarakani.