AFRIKA KUSINI

Julius Malema awasilisha rufaa yake kwa kamati ya nidhamu ya chama cha ANC

Kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama cha ANC aliyesimamishwa uanachama Julius Malema
Kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama cha ANC aliyesimamishwa uanachama Julius Malema REUTERS/Siphiwe Sibeko

Rais wa Umoja wa Vijana wa Chama Tawala nchini Afrika Kusini ANC Julius Malema ambaye kwa sasa amesimamishwa uanachama kwa kipindi cha miaka mitano amewasilisha rufaa yake kisheria kupinga adhabu aliyopewa.

Matangazo ya kibiashara

Malema aliingia hatiani baada ya Kamati ya Nidhamu ya Chama Cha ANC kumkuta na hatia ya kutoa maneno ya kichochezi ya kutaka wananchi wa Botswana waipindue serikali iliyopo madarakani.

Chama Cha ANC kupitia viongozi wake wameshindwa kuthibitishwa kuwasilishwa kwa rufaa hiyo lakini Malema mwenyewe na wafuasi wake wamesema wameshatekeleza hilo kwani wanaamini adhabu iliyotolewa haikuwa halali.

Toka kusimamishwa uanachama kwa Malema kumekuwa na hofu ya kuzuka kwa maandamano ya vijana wa chama cha ANC kupinga hukumu aliyopewa kiongozi wao lakini hata hivyo mpaka sasa imeonekana kuwa hali imetulia.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa huenda rufaa hiyo isiposikilizwa na kutendewa haki kukazuka maandamano makubwa ya vijana nchini humo kupinga maamuzi ya kamati ya nidhamu ya chama hicho kumfungia Malema.