CAIRO-MISRI

Wanaharakati nchini Misri waitisha maandamano zaidi

Waandamanaji wakiwa kwenye uwanja wa Tahrir
Waandamanaji wakiwa kwenye uwanja wa Tahrir Reuters

Wanaharakati nchini Misri wameitisha maandamano makubwa baada ya Sarat Ijumaa kushinikiza utawala wa kijeshi chini ya Field Marshal Mohamed Hussein Tantawi ukae kando wakati Kamal Ganzouri akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyewahi kuhudumu chini ya Rais Hosni Mubarak amekabidhiwa jukumu la kuhakikisha anaongoza mchakato wa uchaguzi kabla ya utawala wa kiraia kuingia madarakani.

Duru za kitabibu zinasema watu arobaini na mmoja wamepoteza maisha nchini humo tangu kuanza kwa maandamano ya kutaka serikali ya kiraia.

Maandamano hayo yankuja wakati ambapo baraza la kijeshi nchini humo lilitangaza kuwa litaachia madaraka kwa serikali ya kiraia mara baada ya uchaguzi mkuu wa Urais uliopangwa kufanyika hapo mwakani.

Juma hili pia baraza hilo lilitangaza kuwa uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika juma lijalo uko palepale na kwamba maandalizi yote yamekwishakamilika kwaajili ya uchaguzi huo.

Hapo jana baraza hilo la kijeshi kwa mara ya kwanza lilitangaza kuomba radhi kwa wananchi pamoja na familia ambazo zimepoteza ndugu zao kutokana na maandamano hayo yaliyoanza ijumaa iliyopita na kuahidi kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuwa waliwaua raia kimakosa.