SOMALIA-MAREKANI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN ataka wanajeshi wa kulinda amani waongezwe nchini Somalia

Reuters路透社

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amesema Vikosi zaidi kwa Kimataifa vinahitajika nchini Somalia kuisaidia Serikali dhaifu ya Rais Sheikh Sharrif Ahmed inayokabiliana na Wanamgambo wa Al Shabab.

Matangazo ya kibiashara

Ban amesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN linapaswa kuongeza nguvu kwa Vikosi vya Umoja wa Afrika AMISOM ambavyo vinashika doria nchini Somalia kwa sasa licha ya kukabiliwa na hali ngumu kutokana na uchache wake.

Katibu Mkuu wa UN amesema wakati umefika sasa kwa Umoja wa Afrika AU na AMISOM kuendelea kuongeza wanajeshi zaidi ili waweze kufikia elfu ishirini badala ya sasa ambapo kuna wanajeshi elfu kumi na mbili pekee.

Kauli ya Katibu Mkuu Ban inakuja wakati ambapo mara kadhaa nchi za Kiafrika zimekuwa mstari wa mbele kulishinikiza Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua y kushika doria nchini Somalia.

Ban ambaye mwishoni mwa juma alitembelea nchini Somalia akiwa ameambatana na Rais wa Bunge la Umoja wa Mataifa UN Nassir Abdulaziz Al Nasser ambaye aliahidi kuketi na Umoja wa Afrika AU kuangalia upya jukumu la kushika doria huko Somalia.

Katibu Mkuu Ban aliweka bayana kuwa serikali ya mpito nchini Somalia inastahili kufikia kikomo mwaka ujao ili kutoa nafasi kwa serikali ya kidemokrasia kuundwa na kumaliza machafuko ya muda mrefu.

Ban ameongeza kuwa amewashauri Viongozi wa serikali ya Mpito kuhakikisha wanaharakisha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya na mabadiliko ya bunge la nchi hiyo vitu ambavyo havihitaji pesa bali utayari wa kisiasa.