JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-DRC

Upinzani Nchini DRC waitisha maandamano ya amani

AFP PHOTO/Junior KANNAH

Upinzani Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC umeitisha maandamano makubwa ya nchi nzima kwa lengo la kupinga matokeo ya Uchaguzi yaliyomrejesha madarakani Rais Joseph Kabila Kabange.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi Mkuu wa Upinzani Etienne Tshisekedi ambaye anadai ameibiwa kura kwenye uchaguzi huo wa rais amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kupaza sauti zao dhidi ya wizi wa kura uliofanyika.

Tshisekedi anaituhumu Tume Huru ya Uchaguzi CENI imetangaza matokeo ambayo si ya kweli na kumpa ushindi Rais Kabila huku akiweka wazi uchaguzi huo kutawaliwa na dosari zinazofanya uchaguzi huo kuwa batili.

Katibu mkuu wa Chama Cha UDPS Jacquemin Shabani amesema maandamano ambayo wameyaitisha ni ya amani na ya kidemokrasia wakiwana na nia ya kutaka kilio chao kisikike na jumuiya ya kimataifa.

Maandamano hayo yanakuja wakati ambapo Umoja wa Ulaya EU, Kituo cha Carater na Waangalizi wengine wa Uchaguzi huo wakisema kulikuwa na mapungufu mengi ambayo yanachangia kuhoji uhalali wa matokeo ya uchaguzi wenyewe.

Nayo serikali ya Marekani imeungana na waangalizi hao kukosoa namna ambavyo uchaguzi huo umefanyika wakidai dosari ambazo zimetajwa zinatosheleza kabisa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais.

Naibu Waziri wa Masuala ya Afrika Bruce Wharton ndiye ambaye ametoa msimamo wa nchi ya Marekani wakitaka serikali kuangalia na kusikiliza malalamiko ambayo yametolewa na waangalizi.

Rais Kabila mapema juma hili akizungumza na wanahabari alikiri uwepo wa mapungufu lakini akasema hiyo ni kawaida kwenye uchaguzi wowote duniani na haiwezi kuwa tiketi ya kubatilisha matokeo yaliyotangazwa na CENI.