Misri

Spika mpya wa Bunge la Misri achaguliwa na vyama vyenye nguvu nchini humo

Vyama vyenye nguvu nchini Misri vya Muslim Brotherhood na Freedom and Justice ambavyo ndivyo vyenye ushawishi mkubwa wa kisiasa vimeafikiana kumchagua Saad Al Katatni kuwa Spika wa Bunge.

Matangazo ya kibiashara

Ni uamuzi ambao ulitangazwa na mwenyekiti wa chama cha Freedom and Justice Mohamed Mursi ambaye amewaambia waandishi wa habari kuwa hatua hiyo imekuja baada ya vyama hivyo viwili kukubaliana kwa kauli moja.

Wananchi wa Misri wamekuwa na shauku kubwa ya kuona serikali mpya inaundwa nchini humo baada ya kuangushwa kwa utawala wa rais Hosni Mubarak ambapo sasa kwa mara ya kwanza wananchihao wametumia demokrasia kuchagua wabunge na wawakilishi.

Kufuatia kupatikana kwa spika mpya wa bunge la nchi hiyo, kikao cha kwanza cha bunge hilo kinatarajiwa kuanza siku ya jumatatu huku masuala mbalimbali yakitarajiwa kujadiliwa ikiwemo uchaguzi mkuu wa urais na uundwaji wa serikali ya kiraia.

Wakati huohuo hii leo mahakama kuu nchini humo inatarajiwa kuendelea kusikiliza kesi inayomkabili Hosni Mubarak na wanawe ambapo jaji anayesikiliza kesi hiyo ameutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi wao hii leo bila kipingamizi.