SOMALIA

Ofisi ya Umoja wa Mataifa UN yafunguliwa nchini Somalia baada ya miaka 17

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN nchini Somalia hatimaye amehamia rsmi katika Mji Mkuu Mogadishu ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kumi na saba tangu Jumuiya ya Kimataifa uanze kuisaidia serikali kupambana na Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab.

Matangazo ya kibiashara

Ofisi za Mjumbe wa Umoja wa Mataifa UN zilikuwepo nchini Kenya tangu mwaka 1995 kutokana na suala la usalama licha ya baadhi ya maofisa wake kuendelea kuwepo Mogadishu kufanya baadhi ya majukumu yao.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN Balozi Augustine Mahiga amewasili Mogadishu rasmi na kupandishwa kwa bendera za UN kwenye ofisi hizo ikiwa ni mwanzo wa shughuli zake.

Ofisi hizi zinafunguliwa mwaka huu wakati nchi hiyo inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu kumaliza kipindi cha serikali ya mpito ambayo imekuwa ikikabiliwa na wakati mgumu kutoka kwa Wanamgambo wa Al Shabab.

Kurejea kwa shughuli za Umoja wa Mataifa UN katika Mji Mkuu Mogadishu kumekuja baada ya kufanikiwa kufurushwa kwa wanagambo wa Al Shabab kutoka katika mji huko mwezi August.

Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Afrika AMISOM kwa kushirikiana na yake ya Serikali yalifanikiwa kuwarudisha nyuma Wanamgambo wa Al Shabab ambao walikuwa wanashiklia eneo kubwa la Mogadishu.

Balozi Mahiga baada ya kuwasili Mogadishu anatarajiwa kukutana na Rais Sheikh Sharif Ahmed pamoja na Maofisa wa Jeshi la Umoja wa Afrika AMISOM kuangalia suala la usalama litadhibitiwa vipi.