Misri

Uhusiano wa Misri na Marekani wahofiwa kuyumba kufuatia uamuzi wa Misri kutaka kuwafungulia Mashtaka wanaharakati wa Marekani

Kiongozi wa serikali ya kijeshi nchini Misri, Hussein Tantawi
Kiongozi wa serikali ya kijeshi nchini Misri, Hussein Tantawi

Maseneta watatu wa Marekani wameitahadharisha Misri kuwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili huenda ukaingia dosari wakati huu kufuatia kuongezeka kwa kasi kwa mashtaka yanayopangwa kutekelezwa dhidi ya wanaharakati wa Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Tahadhari hiyo ambayo imesindikizwa na kiitikio cha hasira kutoka kwa wabunge wa Marekani, maseneta wa chama cha Republican John McCain na Kelly Ayotte wakiungwa mkono na Joe Lieberman pia wameonya kuwa kuendelea kuisaidia Misri ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa msaada wa kifedha ni hatari kwa nchi hiyo.
 

Kwa sasa Marekani inatoa kiasi cha dola bilioni 1.3 kwa mwaka kuisaidia Misri ambayo ni mshirika wake mkubwa katika mataifa ya kiarabu , kiasi ambacho ni kikubwa zaidi kutolewa kwa taifa lolote.
 

Katika taarifa ya pamoja ya Maseneta hao wamesema kuwa mzozo unaoendelea sasa baina yao na serikali ya Misri umeongezeka kwa kiasi kikubwa jambo ambalo linatishia uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo.
 

Majaji wa Misri wametangaza kuwafungulia mashtaka wanaharakati wa masuala ya demokrasia wakiwemo wamarekani 19 kwa madai ya kufadhili kinyume na sheria mashirika ya misaada ya kigeni hatua ambayo imewakasirisha wabunge wa Marekani.