MALI

Spika wa Bunge Nchini Mali ajiandaa kuchukua nafasi ya kuongoza Serikali ya Mpito kabla ya kufanyika Uchaguzi

Spika wa Bunge Nchini Mali Diouncounda Traore ambaye anasubiriwa kuchukua jukumu la kuongoza serikali ya mpito
Spika wa Bunge Nchini Mali Diouncounda Traore ambaye anasubiriwa kuchukua jukumu la kuongoza serikali ya mpito REUTERS/Joe Penney

Spika wa Bunge la Mali Dioncounda Traore anajiandaa kuchukua nafasi ya kuongoza serikali ya mpito kabla ya kuitisha uchaguzi kumaliza vuguvugu la mapinduzi ya kijeshi lililotekelezwa kwa amani katika nchi hiyo kipindi hiki ambapo waasi wa Tuareg wakijitangazia uhuru wa nusu ya nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Spika wa Bunge Traore anatarajiwa kuchukua madaraka ya kuongoza serikali ya mpito kabla ya kuitisha uchaguzi katika kipindi cha siku arobaini tangu aingie madarakani lakini lazima taratibu za kisheria zichukue mkondo wake ndipo aweze kuingia Ikulu kumaliza utawala wa Kijeshi ulioingia madarakani tarehe 22 ya mwezi march.

Kiongozi huyo wa Bunge anatarajiwa kuongoza mchakato wa kidemokrasia katika kurejesha utulivu katika nchi ya Mali ambayo imekumbwa na mgawanyiko mkubwa baina ya eneo la Azawad na Bamako kutokana na kila upande kutaka Utawala wao utambulike rasmi Jumuiya ya Kimataifa.

Mahakama ya Katiba nchini humo kwa upandr wake bado haijaridhia makubaliano ambayo yamefikiwa baina ya Utawala wa Kijeshi unaongozwa na Keptein Amadou Haya Sanogo na Rais Amadou Toumani Toure ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo ili kuruhusu serikali ya Mpito kabla ya kuitisha Uchaguzi.

Hali hiyo inatajwa huenda ikachangia utata wa kisheria na hivyo serikali ya Mpito isitambuliwe Kikatiba na hivyo kulazimisha kurejea madarakani kwa Rais Toure ambaye alitangaza kujiuzulu baada ya makunguzmo yaliyofanywa chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi ECOWAS kukubaliwa na pande zote.

Rais Toure alilazimika kuchukua uamuzi huo ili kama sehemu ya kuhakikisha utulivu na amani unarejea katika nchi yake ambayo imekumbwa na mgawanyiko mkubwa tangu kutekelezwa kwa mapinduzi yasiyomwaga damu ya Jeshi la Nchi hiyo ambalo lilituhumi serikali kwa kushindwa kupambana na Waasi wa Tuareg.

Tayari Kiongozi wa Kijeshi Keptain Sanogo amesema licha ya kuweka kwa makubaliano hayo lakini hawatokaa kimya watakapoona mwenendo wa serikali hauendani na kile ambacho kimeafikiwa chini ya mwamvuli wa ECOWAS.

Haya yanakuja wakati huu ambapo Waasi wa Tuareg wakiwa wameimarisha vyema ngome yao katika eneo la Azawad ambalo wamelitangazia uhuru wake licha ya kukumbana na kikwazo kutoka Jumuiya ya Kimataifa inayopinga hatua iliyofikiwa na MNLA.