MALI

Wanajeshi watiifu kwa Rais aliyepinduliwa Nchini Mali Toure wapambana na Utawala wa Kijeshi

Rais wa serikali ya mpito nchini Mali Dioncounda Traoré akiwa na Kiongozi wa Mapinduzi Kepteni Amadou Haya Sanogo.
Rais wa serikali ya mpito nchini Mali Dioncounda Traoré akiwa na Kiongozi wa Mapinduzi Kepteni Amadou Haya Sanogo. AFP/HABIBOU KOUYATE

Utawala wa Kijeshi nchini Mali ambao ulifanya mapinduzi majuma matano yaliyopita yamejigamba kuweka kwenye himaya yao maeneo muhimu katika Jiji la Bamako baada ya kutokea mapigano makali baina yao na wanajeshi watiifu kwa Rais aliyepinduliwa Amadou Toumani Toure. Ujumbe wa Utawala wa Kijeshi ambao umetolewa kwenye Televisheni ya Taifa umeeleza kuwa wamefanikiwa kuweka chini ya himaya yao Jengo la Utangazaji, Uwanja wa Ndege na Kambi ya Kijeshi ya Kati iliyopo karibu na Mji Mkuu Bamako.

Matangazo ya kibiashara

Utawala wa Kijeshi umesema kuwa kuna kila dalili wanajeshi hao watiifu kwa Rais aliyeondolewa Toure wanapata uungwaji mkono kutoka mataifa ya nchi ili wafanikishe kurejea madarakani kwa kiongozi huyo ambaye ameomba hifadhi nchini Cote D'Ivoire kwa sasa.

Mashambulizi makali baina ya Utawala wa Kijeshi na wanajeshi watiifu kwa Toure yalitokea katika Jengo la Radio na Televisheni ya Taifa, Uwanja wa Ndege na kwenye kambi anayoishi Kapteni Amadou Haya Sanogo.

Utawala wa Kijeshi umesema unawashikilia wanajeshi kadhaa ambao wameongoza makabiliano hayo hukun tetesi za uwepo wa vifo zikiendelea kuzagaa lakini hakuna upande ambao umekuwa tayari kuweka bayana hizo takwimu.

Kepteni Sanogo ameendelea kusisitiza kuwa vikosi vyake ndivyo ambavyo vinashikilia maeneo yote muhimu ikiwemo Vituo vya Radio na Televisheni ya Taifa, Uwanja wa Ndege pamoja na kambi za kijeshi.

Mashuhuda wa mapigano hao wamesema chanzo chake ni hatua ya Utawala wa Kijeshi kutaka kuwakamata walinzi wa zamani wa Rais Toure kitu ambacho kiliwafanya wajihami kwa kutumia silaha na hivyo kuchangia kuzuka kwa makabiliano hayo.

Mapigano haya yamerejesha upya hali ya wasiwasi katika nchi hiyo kipindi hiki ambacho serikali ya mpito imeeanza harakati zake za kuhakikisha inaitisha uchaguzi na hatimaye kurejesha utawala wa kiraia.

Mapinduzi ambayo yalifanyika nchini Mali na kusababisha kuanguka kwa serikali ya Rais Amadou Toumani Toure yalikutana na upinzani mkubwa kutoka Jumuiya ya Kimataifa kitu ambacho kilichangia kuchaguliwa kwa serikali ya Mpito.

Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ndiyo ilikuwa mstari wa mbele kusimamia mazungumzo yaliyoongozwa na Rais wa Burkina Faso Blaise Compaore na hatimaye Spika wa zamani wa Bunge Dioncounda Traore akateuliwa kuwa Rais wa serikali ya Mpito.