MISRI

Waandamanaji tisa wauawa nchini Misri baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha wakiwa nje ya Wizara ya Ulinzi

Waandamanaji nchini Misri wakiwa wameweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi wakishinikiza mwisho wa Utawala wa Kijeshi
Waandamanaji nchini Misri wakiwa wameweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi wakishinikiza mwisho wa Utawala wa Kijeshi

Watu tisa wamepoteza maisha nchini Misri baada ya watu wenye silaha kuwashambulia mamia ya waandamanaji waliopiga kambi nje ya Wizara ya Ulinzi kwa siku kadhaa sasa wakishinikiza kikomo cha Utawala wa Kijeshi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Duru za Wizara ya Ulinzi na Afya kwa pamoja zimethibitisha kutokea kwa vifo hivyo lakini haijabainika ni kina nani ambao wametekeleza mashambulizi hayo ambayo yamesababisha watu kadhaa kujeruhiwa.

Shirika la Utangazaji Nchini Misri MENA limethibitisha watu tisa kupoteza maisha wakati huu ambapo jeshi nchini humo likilazimika kuingilia kati kuzima ghasia ambazo zimezuka baada ya shambulizi hilo lililoacha watu zaidi ya hamsini wakijeruhiwa.

Mashambulizi haya yamekuja na kuchangia vifo na majeruhi huku Utawala wa Kijeshi ukiendelea kukutana na ukosoaji mkubwa kwani wananchi wanadai umeshindwa kuongoza nchi hiyo katika misngi sahihi.

Maofisa wa Wizara ya Ulinzi wamesema kuwa watu hamsini wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo ambalo limeongeza hasira kwa waandamanaji ambao wamekuwa mstari wa mbele kushinikiza kumalizwa kwa muda wa Utawala wa Kijeshi.

Waandamanaji hao ambao wanamuunga mkono wanasiasa Hazem Abu Ismail wameweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi tangu jumamosi wakiishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa hatua yake ya kuwazuia wagombe wenye nguvu kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi ujao.

Siku ya jumapili kulizuka mapigano makali baina ya wafuasi wa Abu Ismail na wakazi wa eneo la Abbassiya eneo ambalo Wizara ya Ulinzi lipo ghasia ambao mtu mmoja alipoteza maisha na wengine mia moja na tisa walijeruhiwa.

Maandamano nchini Misri yameendelea kurejea upya baada ya tume ya taifa ya Uchaguzi nchini Misri kutangaza orodha ya wagombea iliyowaondoa wagombea walihudumu kwenye utawala wa Rais Hosni Mubarak.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi mnamo tarehe kumi na nne ya mwezi April ilitangaza kuwazuia wagombea kumi akiwemo Khairat El Shater na Mkuu wa Intelijensia wa zamani Omar Suleiman kitu ambacho kilichangia kuzusha hasira dhidi ya Utawala wa Kijeshi.

Duru la kwanza la Uchaguzi wa Rais nchini Misri linatarajia kufanyika tarehe 23 na 24 ya mwezi May hatua ambayo itamaliza serikali ya mpito ya Kijeshi ambayo iliingia baada ya kuanguka kwa serikali ya Rais Hosni Mubarak.