SUDAN-SUDAN KUSINI

Sudan yataka amani dhidi ya majirani zao Sudan Kusini huku Baraza la Usalama likitoa saa 48 kabla ya kuweka vikwazo

Mwanajeshi wa Sudan Kusini akiwa kwenye doria kwenye eneo lenye utajiri wa mafuta la Heglig
Mwanajeshi wa Sudan Kusini akiwa kwenye doria kwenye eneo lenye utajiri wa mafuta la Heglig Reuters

Serikali ya Sudan imesema inahaha kuhakikisha amani na utulivu dhidi ya majirani zao wa Sudan Kusini inapatikana na hivyo wametoa wito kwa wenzao wa Juba kuwaunga mkono kutekeleza maazimio ya Umoja wa Afrika AU na Umoja wa Mataifa UN ili kufikia suluhu ya mgogoro wao.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Sudan Al Obeid Meruh ndiye ambaye ametangaza utayari wa serikali ya Khartoum kuweka mikakati ya kupata amani na utulivu na wenzao wa Sudan Kusini.

Serikali ya Khartoum imesema huu ni wakati muafaka wa pande hizo mbili zinazosigana kuhakikisha wanamaliza mtafaruku wao wa kugombea mipaka na maeneo yenye utajiri wa mafuta uliochangia mashambulizi baina yao.

Uamuzi wa Sudan kutaka ipatikane amani baina yao na Sudan Kusini inakuja wakati huu ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN zikitoa saa 48 kwa nchi hizo kuhakikisha wanamaliza uhasama wao wa kugombea mipaka.

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN pamoja na Urusi na China wameunga mkono azimio la kuziwezeka vikwazo nchi za Sudan na Sudan Kusini iwapo zitashindwa kupata suluhu katika kipindi hicho cha saa 48.

Waziri wa Masuala ya Baraza la Mawaziri wa Sudan Kusini Deng Alor Kuol amesema nchi yake ipo tayari kumaliza tofauti zao na majirani zao Sudan ili kurejesha uhusiano mwema uliokuwepo sambamba na kujiepusha na vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Karti amesema serikali yake ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Mpatanishi wa Mgogoro wa nchi hizo kutoka Umoja wa Afrika AU Thabo Mbeki.

Mazungumzo baina ya Rais wa Sudan Omar Hassan Al Bashir na mwenzake wa Sudan Kusini Salva Kiir yamekuwa yakivunjika kila mara na kisha kufuatiwa na mapigano ya kijeshi baina ya nchi hiyo jirani.

Mgogoro baina ya Sudan na Sudan Kusini umeendelea kuchochewa na kugombea mipaka pamoja na umiliki wa maeneo yenye utajiri mkubwa wa visima vya mafuta hasa Kordofan, Heglig na Blue Nile.