MISRI

Waandamanaji 20 wauawa nchini Misri baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha wakiwa nje ya Wizara ya Ulinzi

Waandamanaji nchini Misri wakikabiliana na Jeshi baada ya wenzao walioweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi kuuawa
Waandamanaji nchini Misri wakikabiliana na Jeshi baada ya wenzao walioweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi kuuawa REUTERS/Asmaa Waguih

Watu ishirini wamepoteza maisha nchini Misri baada ya watu wenye silaha kuwashambulia mamia ya waandamanaji waliopiga kambi nje ya Wizara ya Ulinzi kwa siku kadhaa sasa wakishinikiza kikomo cha Utawala wa Kijeshi nchini humo tukio linalokuja siku kadhaa kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Urais.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la nchi hiyo linaloongoza nchi hiyo tangu kuangushwa kwa serikali ya Rais Hosni Mubarak lililazimika kuingilia kati kukabiliana na watu hao wenye silaha ambao walifanya mashambulizi dhidi ya Waandamanaji waliopiga kambi tangu siku ya jumamosi.

Utawala wa kijeshi chini ya Field Marshal Mohammed Hussein Tantawi umelazimika kutoa hakikisho jingine kwa wananchi kwa kuwaeleza wapo tayari kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia ambayo itachanguliwa baada ya uchaguzi wa tarehe 24 May.

Tangazo hilo linabatilisha kauli yake ya awali ambayo iliweka bayana lengo lake ni kuacia madaraka kwa serikali ya kiraia mnamo mwezi Juni lakini kutokana na kuongezeka kwa shinikizo wamebadili uamuzi.

Idadi hiyo ya vifo imethibitishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo imesema watu ishrini ndiyo ambao wamepoteza maisha kwenye mapambano hayo baina ya waandamanaji na watu hao wenye silaha.

Wagombea wanne wa nafasi ya urais nchini Misri wamelazimika kusitisha kampeni zao kutoa nafasi ya maombolezo baada ya kutokea kwa vifo hivyo vilivyongeza wasiwasi juu ya hali ya usalama.

Wagombea ambao wametangaza kusitisha kampeni zao ni pamoja na Abdel Moneim Abul Fotouh, Khaled Ali, Hamdeen Sabbahi na Amr Mussa ambao wamesema wameguswa na hivyo ambavyo vimetokea.

Mashambulizi haya yamekuja na kuchangia vifo na majeruhi huku Utawala wa Kijeshi ukiendelea kukutana na ukosoaji mkubwa kwani wananchi wanadai umeshindwa kuongoza nchi hiyo katika misngi sahihi.

Maofisa wa Wizara ya Ulinzi wamesema kuwa watu hamsini wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo ambalo limeongeza hasira kwa waandamanaji ambao wamekuwa mstari wa mbele kushinikiza kumalizwa kwa muda wa Utawala wa Kijeshi.

Waandamanaji hao ambao wanamuunga mkono wanasiasa Hazem Abu Ismail wameweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi tangu jumamosi wakiishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa hatua yake ya kuwazuia wagombe wenye nguvu kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi ujao.

Siku ya jumapili kulizuka mapigano makali baina ya wafuasi wa Abu Ismail na wakazi wa eneo la Abbassiya eneo ambalo Wizara ya Ulinzi lipo ghasia ambao mtu mmoja alipoteza maisha na wengine mia moja na tisa walijeruhiwa.

Maandamano nchini Misri yameendelea kurejea upya baada ya tume ya taifa ya Uchaguzi nchini Misri kutangaza orodha ya wagombea iliyowaondoa wagombea walihudumu kwenye utawala wa Rais Hosni Mubarak.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi mnamo tarehe kumi na nne ya mwezi April ilitangaza kuwazuia wagombea kumi akiwemo Khairat El Shater na Mkuu wa Intelijensia wa zamani Omar Suleiman kitu ambacho kilichangia kuzusha hasira dhidi ya Utawala wa Kijeshi.

Duru la kwanza la Uchaguzi wa Rais nchini Misri linatarajia kufanyika tarehe 23 na 24 ya mwezi May hatua ambayo itamaliza serikali ya mpito ya Kijeshi ambayo iliingia baada ya kuanguka kwa serikali ya Rais Hosni Mubarak.